China yafanya shughuli za kumbukumbu ya miaka 89 tangu kuanza kwa vita dhidi ya uvamizi wa Japan (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 08, 2026
China yafanya shughuli za kumbukumbu ya miaka 89 tangu kuanza kwa vita dhidi ya uvamizi wa Japan
Hafla ya kumbukumbu ya miaka 89 tangu kuanza kwa vita vya mapambano ya nchi nzima ya China dhidi ya uvamizi wa Japan ikifanyika katika Jumba la Makumbusho ya Vita vya Watu wa China vya Kupambana na Uvamizi wa Japan mjini Beijing, Julai 7, 2026. (Xinhua/Zhang Ling)

BEIJING/TAIPEI – Jana Jumanne China imefanya shughuli za kumbukumbu ya miaka 89 tangu kuanza vita vya nchi nzima vya kupambana na uvamizi wa Japan, ambapo ilipiga kengele ya amani na kutoa onyo kwa wamilitarism wapya wa Japan.

Ingawa uvamizi wa Japan dhidi ya China ulianza mapema mwaka 1931, katika Tukio la Julai 7 mwaka 1937, jeshi la Japan liliwashambulia wanajeshi wa China waliolinda kitongoji cha Beijing. Tukio hilo liliashiria kupamba moto kwa uvamizi huo wa Japan hadi kuwa uvamizi dhidi ya China wa pande zote, na pia kuonesha mwanzo wa mapambano ya China ya nchi nzima dhidi ya uvamizi huo.

Huku shughuli za kumbukumbu zikifanyika kote nchini China, maofisa na wasomi wa China wamesisitiza umuhimu wa nyakati za sasa wa shughuli hizo za kitaifa, hasa kutokana na vitendo mfululizo vya uchokozi vilivyofanywa hivi karibuni na Japan. Vitendo hivyo ni pamoja na kurahisisha vizuizi vya mauzo ya nje ya silaha kali, na kuashiria hadharani huenda itafanya uingiliaji kati kijeshi wakati wa kutokea "hali ya dharura" ya Taiwan -- eneo lililokuwa koloni la Japan kwa nusu karne.

Mjini Beijing, hafla imefanyika katika Jumba la Makumbusho ya Vita vya Watu wa China vya Kupambana na Uvamizi wa Japan karibu na Daraja la Lugou, ambako tukio la Julai 7 lilitokea miaka 89 iliyopita.

Yin Li, mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na katibu wa Kamati ya CPC ya Mji wa Beijing aliongoza hafla hiyo. Washiriki wa shughuli walitoa maua na kuinama ili kutoa heshima na kuwaenzi wale waliojitolea maisha yao katika kupambana na uvamizi wa Japan.

Katika sehemu mbalimbali nchini China, wanafunzi walikusanyika kwenye majumba ya makumbusho ili kufahamishwa tukio la kihistoria, na watu waliweka maua katika majumba ya kumbukumbu. Mjini Nanjing, kengele ya amani ilipigwa kwenye Jumba la Kumbukumbu ya Wahanga katika Mauaji Makubwa ya Nanjing Yaliyofanywa na Wavamizi wa Japan.

Huko Taiwan, shughuli mfululizo za kumbukumbu zimefanyika siku hiyo ya Jumanne. Katika shughuli moja iliyoanzishwa na vyama kadhaa vya kisiasa na makundi ya kiraia huko Taoyuan, waandaaji wamesema historia ya pamoja ya mapambano dhidi ya uvamizi wa Japan si tu ni kumbukumbu ya pamoja ya taifa la China, bali pia imekuwa ukurasa muhimu katika historia ya Taiwan ya kupinga utawala wa kikoloni wa Japan, na kuwa msingi muhimu wa amani na kuaminiana kwa pande mbili za Mlango-Bahari.

Kwa watu wa China, Tukio la Julai 7 linabaki kuwa tukio lisilosahaulika katika Vita vya Pili vya Dunia kama ilivyo kwa matukio ya uvamizi wa Blitzkrieg uliofanywa na Nazi ya Ujerumani nchini Poland na shambulio la kushtukiza la Japan kwenye Bandari ya Pearl kwa nchi za Magharibi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha