Lugha Nyingine
China itaendelea kuzisaidia nchi za Afrika katika kupambana na Ebola
BEIJING - Lin Jian, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China amesema kwamba, kwa kuwa mlipuko wa Ebola bado unaenea barani Afrika, China itaendelea kuzisaidia nchi za Afrika na kutoa uungaji mkono unaohitajika ili mlipuko huo uweze kukomeshwa mapema iwezekanavyo.
Lin ameyasema hayo jana Jumanne alipokuwa akijibu swali kuhusu timu ya tatu ya wataalamu wa matibabu iliyotumwa na serikali ya China iliyofika Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Agosti 1.
Amesema kwamba baada ya mlipuko wa Ebola kutokea barani Afrika, China imetilia maanani sana hali hiyo na kutuma timu mbalimbali za wataalamu wa matibabu katika nchi zinazoathirika, ikiwemo DRC, ili kupambana na mlipuko huo, jambo ambalo limepongezwa sana.
Lin ameeleza kuwa timu hiyo ya tatu ya wataalamu wa matibabu inaundwa na wataalamu wa magonjwa ya mlipuko, karantini ya afya, matibabu ya magonjwa, na upimaji wa vimelea ndani ya maabara. Amesema, kwenye msingi wa kazi zilizofanywa na timu zilizopita, timu hiyo itaendelea kuimarisha hali ya kubadilishana maoni na kufanya uratibu na DRC na mashirika ya kimataifa kutokana na mahitaji ya kuzuia na kudhibiti maambukizi ya ugonjwa.
"Kwa kuwa mlipuko wa Ebola bado unaenea, China itaendelea kupeleka wataalamu wake wa matibabu barani humo, kusaidia nchi za Afrika na kutoa uungaji mkono unaohitajika ili mlipuko huo ukomeshwe mapema iwezekanavyo," Lin amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



