Lugha Nyingine
China yatangaza kigezo cha usalama kwa mifumo ya kujiendesha ya magari

Teksi ya Pony.ai inayojiendesha yenyewe ikionekana katika Eneo la Nanshan la Shenzhen, Mkoa wa Guangdong, kusini mwa China, Machi 28, 2026. (Xinhua/Liu Mengqi)
BEIJING - China imetangaza kwa umma kigezo cha lazima cha kitaifa kuhusu mahitaji ya usalama kwa mifumo ya kujiendesha ya magari, Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Kupashana Habari ya China (MIIT) imesema jana Jumanne.
Kigezo hicho, kilichoidhinishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Soko ya Serikali ya China na Mamlaka ya Kitaifa ya China ya Uwekaji Vigezo, kimepangwa kuanza kutumika Julai 1, 2027.
Wizara hiyo imesema, kigezo hicho kinatumika kwa vyombo vya usafiri vya kategoria ya M na N vyenye mifumo ya kujiendesha ya Ngazi ya 3 na Ngazi ya 4, lakini hakijumuishi mifumo ya kuegesha kiotomatiki.
Imeeleza kwamba kiwango hicho kinawataka watengenezaji wa magari kuboresha mifumo ya uhakikisho wa usalama katika mzunguko mzima wa matumizi ya bidhaa na kufanya majaribio ya kuigilizia hali halisi, ya vitendo na ya barabarani wakati wa uundaji na uthibitishaji wa mifumo hiyo ya kujiendesha.
Pia kinataka uwezo imara zaidi katika kutekeleza majukumu ya uendeshaji yanayohitaji mwitiko wa wakati halisi, huku kikibainisha mahitaji ya mwingiliano kati ya binadamu na mashine na arifu kwa mtumiaji ili kuzuia matumizi mabaya na yasiyofaa.
Kwa mifumo ya Ngazi ya 3, vyombo vya usafiri lazima viweze kufuatilia utayari wa madereva wa kuchukua udhibiti.
Kwa kutazama siku za baadaye, wizara hiyo imesema kwamba itaimarisha usimamizi wa upatikanaji sokoni kwa bidhaa za vyombo vya usafiri vilivyounganishwa na mifumo ya AI, kuboresha mbinu za upimaji kwa mifumo ya vyombo vya usaifiri kujiendesha vyenyewe, na kujenga utaratibu mzuri wa usimamizi kwa vyombo vya usafiri vilivyounganishwa na mifumo ya AI ili kuhakikisha maendeleo yenye sifa bora ya sekta hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



