Lugha Nyingine
Waziri wa Afrika Kusini atoa wito wa mbinu ya pamoja ya bara juu ya uhamiaji
JOHANNESBURG - Afrika Kusini imetoa wito wa kutekeleza uamuzi wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu kuitisha mkutano wa bara zima ili kushughulikia vyanzo vinavyosababisha uhamiaji na changamoto zinazohusiana na uhamiaji usiofuata taratibu, Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa nchi hiyo Ronald Lamola amesema.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Pretoria jana Jumatano, Lamola amesema uhamiaji ni jambo la bara zima ambalo linahitaji mwitikio kamili na wa pamoja badala ya majadiliano yanayolenga nchi moja pekee.
Kauli zake hizo zinafuatia uamuzi wa Mkutano wa 49 wa Kawaida wa Baraza la Utendaji la AU kutojadili uhamiaji katika mkutano ujao wa mapitio ya katikati ya mwaka wa AU.
Lamola amesema Afrika Kusini iliendelea kuunga mkono utekelezaji wa azimio lililopitishwa kwenye Mkutano Mkuu wa 25 wa AU mjini Johannesburg mwaka 2015, ambalo ulitoa wito wa kuitishwa mkutano wa Afrika juu ya uhamiaji.
Amesema mkutano huo uliopendekezwa unapaswa kuzingatia njia za kuharakisha uhamiaji wa watu na maendeleo ndani ya Afrika huku ukishughulikia ongezeko la uhamiaji usiofuata taratibu na kuimarisha uwezo wa bara hilo kudhibiti mtiririko wa uhamiaji.
Lamola amesema majadiliano juu ya uhamiaji yanapaswa kushughulikia vyanzo vyake na mambo yanayochangia, yakiwemo ya mabadiliko ya tabianchi, hali za kiuchumi, amani na utulivu, utawala wa kidemokrasia na mafungamano ya kikanda.
Lamola amesema mkutano huo unapaswa pia kuwezesha nchi za Afrika kujadili vyanzo vinavyosababisha hisia za kupinga wahamiaji na kuandaa mbinu ya pamoja wa bara ili kuzuia vurugu, ubaguzi, chuki dhidi ya wageni na aina nyingine za kutovumiliana.
Lamola amesema AU inapaswa kufufua utekelezaji wa azimio hilo lililopitishwa mwaka 2015 badala ya kuchukulia uhamiaji kama suala la kipekee kwa Afrika Kusini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



