Lugha Nyingine
Afrika Kusini yaadhimisha miaka 70 ya Maandamano ya Wanawake ya kihistoria
PRETORIA, Afrika Kusini - Afrika Kusini imeadhimisha Siku ya Wanawake ya Kitaifa kwenye Majengo ya Muungano huko Pretoria, mji mkuu wa utawala wa nchi hiyo, ikiadhimisha miaka 70 ya Maandamano ya Wanawake ya kihistoria ya mwaka 1956, wakati wanawake wapatao 20,000 walipoandamana hadi kwenye makao ya utawala kupinga sheria ya ubaguzi wa rangi kwenye usafiri dhidi ya wanawake.
Akihutubia maadhimisho hayo ya kitaifa yaliyofanyika jana Jumapili, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametoa heshima kwa wanawake walioshiriki kwenye maandamano hayo ya mwaka 1956 na kusisitiza jukumu lao kwenye mapambano ya muda mrefu ya nchi hiyo dhidi ya ubaguzi wa rangi na usawa wa kijinsia.
"Wanawake hao wa mwaka 1956 walikuwa wakipinga vitambulisho vya ubaguzi wa rangi kwenye usafiri dhidi ya wanawake, lakini ujumbe wao ulifikia mbali zaidi ya sheria ya vitambulisho hivyo. Walipambana na mtazamo kwamba wanawake wanapaswa kufungiwa nyumbani, kuwa kimya katika mambo ya umma, na kuwa chini ya wanaume," Ramaphosa amesema.
Agosti 9, 1956, wanawake takriban 20,000 kutoka kote Afrika Kusini walikusanyika kwenye Majengo ya Muungano kupinga serikali ya ubaguzi wa rangi kupanua sheria ya ubaguzi wa rangi kwenye usafiri dhidi ya wanawake. Maandamano hayo yaliongozwa na Lilian Ngoyi, Helen Joseph, Rahima Moosa, na Sophia Williams-de Bruyn.
Rais huyo amesema, "Maandamano hayo yalisaidia kubadilisha mchakato, hali na njia ya uongozi wa mapambano ya nchi yetu ya kujipatia uhuru na haki," na yalionyesha kwamba wanawake hawakuwa tu waungaji mkono wa mapambano, bali pia ni viongozi, waandaaji, na wapangaji wake.
Ramaphosa amesema maendeleo makubwa yamepatikana tangu kukomeshwa kwa ubaguzi wa rangi mwaka 1994, akiongeza kuwa wanawake sasa wana haki ya kupiga kura, kuwa maofisa wa umma, kumiliki mali na ardhi, kurithi mali, na kushika nyadhifa za juu katika taasisi za umma za nchi.
Pia amekiri kwamba changamoto kubwa bado zipo, na wanawake wengi bado wanakabiliwa na kutengwa kiuchumi na vizuizi vingine vya kupiga hatua kimaendeleo.
Chini ya kaulimbiu ya mwaka huu, "Kuwapa Haki Wanawake, Kuongeza Uwezo wa Nchi”, shughuli ya maadhimisho ya mwaka huu inasisitiza kuboresha nafasi ya wanawake ya kupata huduma bora za matibabu, hii ni muhimu sana kwa maendeleo endelevu, haki kwenye jamii, na ukuaji wa uchumi.
Siku hiyo ya Wanawake ya Kitaifa imekuwa ikiadhimishwa nchini Afrika Kusini Tarehe 9 Agosti ya kila mwaka tangu mwaka 1994, na ni sehemu moja ya shughuli ya maadhimisho ya kila mwezi ya Wanawake wa nchi hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



