Namna panya wa Tanzania wabobezi wa harufu wanavyo kuwa waokoaji wa maisha wasiotarajiwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 26, 2026
Namna panya wa Tanzania wabobezi wa harufu wanavyo kuwa waokoaji wa maisha wasiotarajiwa
Panya buku wa Afrika akifanya mafunzo ya kuiga ya kutafuta mabomu ya ardhini kwenye kipindi cha mafunzo katika Kituo cha Mafunzo na Utafiti wa Panya wa Kutafuta cha Apopo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro, Tanzania, Agosti 19, 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman)

MOROGORO, Tanzania - Chini ya Milima ya Uluguru mashariki mwa Tanzania, mashujaa wasiotarajiwa wako kwenye mafunzo ya kunusa baadhi ya matatizo magumu zaidi duniani. Kutana na panya buku wa Afrika – wenye umbo dogo lakini kipaji kikubwa cha kunusa.

Kwenye Kituo cha Mafunzo na Utafiti wa Panya wa Kutafuta cha Apopo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro nchini Tanzania, panya hao wanafunzwa kutafuta mabomu yaliyotegwa ardhini, kifua kikuu, bidhaa haramu za wanyamapori na hata watu waliokwama chini ya majengo yaliyoporomoka.

Miongoni mwa wale wanaosaidia kubadilisha uwezo wa asili wa wanyama hao kuwa kifaa cha kuokoa maisha ni mkufunzi Richard Emily, ambaye amekuwa akifanya kazi na panya hao kwa miaka takriban minne pamoja na wakufunzi na watafiti zaidi ya 30 wanaohusika katika miradi tofauti ya Apopo.

"Shauku yangu ni kuwafunza panya hawa kuokoa maisha ya binadamu. Kazi yao haiwezi kuelezeka kwa maneno pekee," amesema Emily, akiwa amevalia fulana yenye maandishi "Apopo inaokoa maisha."

Kituo hicho, kilichopo umbali wa kilomita takriban 200 magharibi mwa mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, Dar es Salaam, ni sehemu ya juhudi pana zaidi za Apopo za kukuza panya wenye uwezo wa kukabiliana na baadhi ya changamoto zinazosumbua zaidi za jamii.

Apopo, ambalo linatokana na kifupi cha sentensi ya Kiholanzi ya "Uendelezaji wa Bidhaa za Kubaini Mabomu ya Ardhini Dhidi ya Watu" ilisajiliwa nchini Ubelgiji mwaka 1997. Mradi huo ulijikita katika kutafuta mabomu ya ardhini kabla ya kupanuka hadi katika utambuzi wa kifua kikuu, utafutaji na uokoaji, na hivi karibuni, biashara haramu ya wanyamapori.

Said Mshana, mratibu wa utafiti na data wa mradi huo wa Apopo katika SUA, amesema wazo la kutumia panya buku wa aina hiyo wa Afrika kwa ajili ya kutafuta lilitoka kwa mhandisi wa bidhaa wa Ubelgiji Bart Weetjens, ambaye mwanzoni alitafuta suluhisho la bei nafuu kwa tatizo la mabomu ya ardhini katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Baada ya kugundua hisia ya ajabu ya kunusa ya panya hao, Weetjens alijiuliza kwa nini wasiweze kufunzwa kutafuta mabomu ya ardhini. Hilo hatimaye lilisababisha utafiti na uundaji wa mfumo kwa ajili ya kuwafunza panya hao.

"Kwa panya wa kubaini mabomu ya ardhini, inachukua miezi takribani tisa hadi mwaka kutoa mafunzo kikamilifu," Mshana amesema.

Hapo SUA, panya wa kubaini wanyamapori tayari wameonyesha matokeo yenye kuleta matumaini kwa kubainisha kwa ufanisi bidhaa haramu za wanyamapori wakati wa mafunzo.

Hatua inayofuata ni kuanza kutumwa kwa ajili ya operesheni, huku kituo hicho cha Apopo kikitarajia kufanya kazi na mamlaka husika kuwaingiza panya hao kwenye maeneo ya kimkakati kama vile bandarini, viwanja vya ndege na vivuko vya mpakani.

Katika kituo hicho hicho, watafiti wanawapa mafunzo ya kubaini mahali walipo watu waliokwama chini ya vifusi kufuatia majanga kama vile matetemeko ya ardhi na maporomoko ya ardhi. Hivi majuzi, panya sita walitumwa Uturuki kwa ushirikiano na shirika la kujitolea la Uturuki GEA ili kuwasaidia watafiti kutathmini ufanisi wao katika mazingira halisi ya kufanya kazi.

Mshana anaamini kwamba Tanzania hatimaye inaweza kuwa kituo cha ubora wa kimataifa cha kuwafunza panya buku hao wa Afrika.

Ustawi wa wanyama unabaki kuwa kipaumbele kikuu. Panya hao hupokea chakula chenye lishe, mazoezi na uchunguzi wa afya mara kwa mara, wakati huohuo saa zao za kazi ni chache ili kuzuia msongo wa mawazo kupita kiasi.

Mmoja wa panya maarufu zaidi wa kituo hicho cha Apopo ni Magawa, panya buku wa Afrika anayejulikana kimataifa baada ya kubaini mabomu mengi ardhini na kupokea medali ya dhahabu kwa mafanikio yake hayo. Magawa alistaafu nchini Cambodia na baadaye akafa.

Leo hii, panya takriban 240 wanahifadhiwa kwenye kituo hicho katika hatua tofauti za mafunzo. Baadhi ya panya wa kubaini kifua kikuu wanafanyiwa mafunzo kwenye kituo kingine cha Apopo jijini Dar es Salaam, huku mipango ikiendelea ya kuanzisha kliniki nyingine ya kubaini kifua kikuu katika jiji la Arusha kaskazini mwa Tanzania.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha