Wanafunzi wa Kenya washiriki kwenye sherehe ya Siku ya Mid-Autumn ya China

(CRI Online) Septemba 18, 2026

Nyimbo, ngoma, sanaa na vyakula vimetawala katika sherehe ya sikukuu ya katikati ya msimu wa mpukutiko (Mid-Autumn) iliyoandaliwa katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Kenyatta. Sherehe hiyo imewaleta pamoja wanafunzi kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari zinazofundisha lugha ya Kichina, huku washiriki wakipata fursa ya kujifunza na kushirikiana katika tamaduni za Kenya na China.

Ndivyo ilivyokuwa katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Kenyatta, ambapo sherehe ya sikukuu hiyo imewaleta pamoja wanafunzi, walimu na wadau wa elimu na utamaduni.

Sherehe hii ya jadi ya China huadhimishwa wakati wa mwezi mpevu, ikiwa ni kipindi kinachohusishwa na umoja, familia, urafiki na mshikamano.

Na kwa wanafunzi wa shule za Kenya wanaojifunza Kichina, ilikuwa fursa ya kuifahamu zaidi tamaduni ya nchi hiyo kwa njia ya vitendo.

Wanafunzi kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari walishiriki katika shughuli tofauti, zikiwemo kuimba nyimbo na kucheza ngoma za jadi za China pamoja na kutazama maonyesho ya utamaduni wa Kenya.

Mchanganyiko huo wa tamaduni wa aina mbili ulifanya hafla hiyo kuwa ya kipekee, huku wanafunzi wakionyesha vipaji vyao na kujifunza kuhusu mila na desturi za wenzao kutoka upande mwingine.

Kwa waandalizi na wazungumzaji katika hafla hiyo, matukio kama haya yana nafasi muhimu katika kujenga uelewano na urafiki kati ya Kenya na China.

Walihimiza kuendelea kwa mabadilishano ya kitamaduni, wakisema kuwa uhusiano kati ya mataifa mawili haupaswi kuishia katika biashara na ushirikiano wa serikali pekee, bali pia kuwahusisha wananchi, hasa vijana.

Kupitia kujifunza lugha, muziki, sanaa na mila za nchi nyingine, vijana wanapata nafasi ya kuifahamu jamii hiyo kwa undani na kuvunja dhana potofu zinazoweza kujengwa kutokana na kutofahamiana.

Kwa wanafunzi wanaojifunza Kichina, sherehe hiyo pia ilikuwa mafunzo nje ya darasa.

Walipata fursa ya kutumia lugha hiyo, kuandika na kuchora herufi za Kichina, huku wengine wakijifunza maana na matumizi ya baadhi ya alama hizo.

Na bila shaka, hakuna sherehe ya sikukuu hiyo inayokamilika bila "moon cake," kitafunwa maarufu kinachohusishwa na tamasha hilo.

Wanafunzi na wageni walipata fursa ya kuonja moon cake na kushiriki katika utamaduni huu wa China.

Miongoni mwa vivutio vilivyofanya hafla hiyo iwe hai ni namna wanafunzi walivyokuwa mstari wa mbele katika maonyesho.

Kuanzia nyimbo za Kichina, ngoma za Kenya, hadi sanaa ya kaligrafia, washiriki walionyesha kwamba utamaduni unaweza kuwa daraja la kuwaunganisha watu wenye asili tofauti.

Na kwa wanafunzi wanaojifunza Kichina katika shule za Kenya, uzoefu kama huu unawapa zaidi ya ujuzi wa lugha — bali pia unawapa nafasi ya kuifahamu China kupitia watu, sanaa na utamaduni wake.

Kwa ujumla, sherehe hiyo ilikuwa jukwaa la furaha, kujifunza na kubadilishana tamaduni, huku ujumbe mkuu ukiwa wazi — kwamba wananchi wa Kenya na China wanaweza kujenga uhusiano wa karibu zaidi kupitia lugha, elimu, sanaa na utamaduni.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha