Lugha Nyingine
Michezo ya Asia | China yatwaa medali za mbio za kupokezana vijiti huku rekodi mbili za Michezo hiyo zikivunjwa

Xie Zhenye, Zeng Keli, Wang Shengjie na Chen Jinfeng (kutoka kushoto kwenda kulia) wa China wakipiga picha baada ya kushinda fainali ya mbio za kupokezana vijiti za mita 4x100 kwa wanaume kwenye Michezo ya Asia 2026, Nagoya, Japan, Septemba 28, 2026. (Xinhua/Luo Yuan)
NAGOYA, Japan - China imeendeleza kampeni yake imara katika mashindano ya riadha kwenye Michezo ya Asia 2026 jana Jumatatu, ikishinda medali nne za dhahabu, zikiwemo mataji yote mawili ya mbio za kupokezana vijiti za mita 4x100 kwa wanaume na wanawake, huku Mariam Kareem wa UAE na Kazuto Iizawa wa Japan wakiweka rekodi mpya za Michezo hiyo.
Kareem, mwenye umri wa miaka 18, ameshinda mbio za wanawake za mita 400 za kuruka viunzi kwa muda wa sekunde 54.31, akivunja rekodi ya awali ya Michezo hiyo ya sekunde 54.45 mjini Hangzhou mwaka 2023, wakati Kong Yingying wa China amemaliza wa nne kwa muda wa sekunde 55.78.
Bassem Hemeida wa Qatar ameshinda mbio za wanaume za mita 400 kuruka viunzi kwa muda wa sekunde 47.82, akifuatiwa na Taiju Goto wa Japan na Lin Chung-wei wa Taipei ya China.
Iizawa pia ameweka rekodi ya Michezo ya Asia, akitumia muda wa dakika 3:36.35 kushinda mbio za wanaume za mita 1,500, wakati Liu Dezhu wa China amemaliza wa nne.
Katika mashindano ya kurusha kisahani (discus) kwa wanawake, Feng Bin wa China ametetea taji lake kwa kurusha umbali wa mita 63.83 katika raundi ya mwisho. Mwanamichezo Mchina mwenzake Jiang Zhichao ameshinda medali ya fedha kwa kurusha umbali wa mita 62.25—matokeo yake bora zaidi msimu huu.

Feng Bin wa China akishiriki kwenye fainali ya kurusha kisahani (discus) kwa wanawake. (Xinhua/Luo Yuan)
Shi Yuhao ameipatia China medali ya pili ya dhahabu katika riadha usiku huo kwenye Uwanja wa Mizuho, akishinda mashindano ya kuruka mbali kwa wanaume kwa umbali wa mita 8.17—matokeo yake bora zaidi msimu huu—katika jaribio lake la pili.

Shi Yuhao akishiriki kwenye fainali ya kuruka mbali kwa wanaume. (Xinhua/Luo Yuan)
Baadaye, China ilinyakua mataji yote mawili ya mbio za kupokezana vijiti za mita 4x100 kwa wanaume na wanawake. Liang Xiaojing, Liu Guoyi, Liu Xiajun na Chen Yujie walishirikiana kushinda mbio za wanawake kwa muda wa sekunde 42.96.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



