Lugha Nyingine
Utaalamu wa kufuga nyuki kutoka China wafungua fursa mpya kwa wanawake wa Kenya

Mwanachama wa kikundi cha wanawake cha Lelkolo akionesha asali katika Kaunti ya Baringo, Kenya, Septemba 15, 2026. (Xinhua/Liu Qiong)
NAIROBI - Grace Cheserem, mwenyekiti wa kikundi cha wanawake cha Lelkolo katika Kaunti ya Baringo, Kenya, bado anakumbuka mavuno yake ya kwanza ya asali mwaka 2022.
Akiwa amevalia kofia yenye wavu wa kujikinga, alifungua mzinga wa nyuki kwa uangalifu, huku karibu sauti pekee aliyoweza kusikia ikiwa pumzi yake mwenyewe. Asali hiyo ya rangi ya dhahabu ilikuwa iking'aa kwenye mwanga wa jua, hali ambayo ilizua shangwe kutoka kwa wanawake waliokuwa wamekusanyika kumzunguka.
Katika jamii za eneo hilo, ufugaji nyuki kwa muda mrefu ulichukuliwa kuwa kazi ya wanaume. Mizinga ya kienyeji mara nyingi iliwekwa juu ya mitini, jambo lililofanya uvunaji wa asali kuwa kazi inayohitaji nguvu nyingi. Kwa sababu hiyo, ufugaji nyuki ulichukuliwa kuwa mwiko kwa wanawake.
Leo hii, kikundi hicho cha wanawake chenye wanachama 21 kimejifunza kusimamia mizinga na kuvuna asali chenyewe, na kimeanza kuendesha biashara yake ya asali.
Mwaka 2025, kikundi hicho kilivuna kilo 612 za asali na kupata shilingi takriban 500,000 za Kenya (dola za Marekani 3,850) kutoka kwenye mauzo.
Mabadiliko hayo yametokana na juhudi za afisa ugani wa kilimo, Aholipama Chelagat Rutto, ambaye alileta wenyeji wa jamii hiyo mbinu za ufugaji nyuki alizojifunza nchini China.

Mwanachama wa kikundi cha wanawake cha Lelkolo akikagua mizinga ya nyuki katika Kaunti ya Baringo, Kenya, Septemba 15, 2026. (Xinhua/Liu Qiong)
Mwaka 2017, Rutto alisafiri hadi Changsha, mji wa katikati mwa China, kushiriki katika programu ya mafunzo kuhusu uzalishaji wa mazao ya nyuki na kuongeza mavuno ya mazao yanayozalisha mafuta, iliyoandaliwa na Wizara ya Biashara ya China na kuendeshwa na taasisi ya sayansi na teknolojia ya kilimo ya mjini humo.
Kabla ya safari hiyo, ujuzi wa Rutto kuhusu ufugaji nyuki ulikuwa wa kinadharia zaidi. "Nilijifunza mambo kadhaa shuleni, kama vile historia, mzunguko wa maisha na tabia za nyuki, lakini sikuwahi kujifunza kwa kina mbinu za ufugaji wa nyuki," amesema.
Akiwa nchini China, alipata mafunzo ya hatua kwa hatua kuhusu ujenzi wa mashamba ya nyuki, uzalishaji wa makundi ya nyuki na usimamizi wa mizinga, pamoja na kujifunza mbinu za kudhibiti wadudu na magonjwa, kutathmini ukomavu wa asali na namna ya kuvuna asali.
Baada ya kurudi Kenya, Rutto alianza kuwaelezea wanawake wenyeji maarifa aliyopata. "Nilitaka wapate ujuzi zaidi na kuwa wenye kujitegemea kiuchumi," amesema.

Wanachama wa kikundi cha wanawake cha Lelkolo wakiimba kwenye eneo la ufugaji nyuki katika Kaunti ya Baringo, Kenya, Septemba 15, 2026. (Xinhua/Liu Qiong)
Rutto alianza kuhamasisha matumizi ya mizinga ya kisasa, ikiwemo mizinga ya aina ya Langstroth, pamoja na mavazi ya kujikinga na zana maalum za ufugaji nyuki.
Kadiri wanawake hao walivyozidi kumudu mbinu za ufugaji nyuki, mabadiliko yalianza pia kuonekana katika kaya zao.
"Wakati wanaume walipoona kuwa tunaweza kufanya kazi hii vizuri, walikubali kabisa," amesema Cheserem. "Sasa mimi na mume wangu tunagawana majukumu ya nyumbani."

Wanachama wa kikundi cha wanawake cha Lelkolo wakivuna asali katika Kaunti ya Baringo, Kenya, Septemba 15, 2026. (Xinhua/Liu Qiong)
"Bila mapato kutoka ufugaji nyuki, maisha yetu yangekuwa magumu sana," amesema Faith Kittony, katibu wa kikundi hicho cha wanawake, akiongeza kuwa ufugaji nyuki umekuwa chanzo cha mapato wanachoweza kutegemea katika kukabiliana na hali ya hewa isiyotabirika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



