Lugha Nyingine
China yatoa miongozo juu ya kuendeleza nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora
BEIJING - Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Baraza la Serikali la China vimetoa seti ya miongozo inayolenga kuharakisha maendeleo ya nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora ili kuhimiza maendeleo yenye sifa bora.
Miongozo hiyo inaelezea hatua 19 muhimu katika maeneo matano, yaani kusukuma mbele uvumbuzi wa sayansi na teknolojia, kuzidisha mafungamano ya sayansi na teknolojia na uvumbuzi wa kiviwanda, kuvumbua mbinu za maendeleo, kuhimiza uvumbuzi wa utaratibu na mifumo, na kukamilisha mfumo wa ukuaji wa vipaji.
Kwa kuzingatia kwamba kuendeleza nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora ni hitaji la msingi na lengo muhimu la kuhimiza maendeleo yenye sifa bora, miongozo hiyo inasisitiza umuhimu wa maendeleo yanayotegemea uvumbuzi, mageuzi na hatua zinazotekelezwa kwa kulingana na hali halisi za maeneo husika, na kufuata mbinu ya "hatua mpya zatekelezwa kabla ya kuacha zile za zamani."
Miongozo hiyo inatoa matakwa ya kutafuta teknolojia ya hali ya juu, ufanisi wa juu na ubora wa juu, kushughulikia ipasavyo uhusiano kati ya serikali na soko, kati ya sifa ya nguvu za uzalishaji na namna zinavyotumika katika viwanda na biashara, kati ya mageuzi na maendeleo, na kati ya kujitegemea na kufungua mlango, na wakati huohuo kuratibu maendeleo na usalama.
Miongozo hiyo inatoa matakwa ya kutekeleza kikamilifu mpango wa "AI Plus", kutumia AI kubadilisha viwanda vya jadi, kuharakisha uvumbuzi katika AI na teknolojia nyingine za kidijitali na teknolojia zenye akili, na kuhimiza matumizi zaidi ya AI katika shughuli zote na viwanda vyote.
Wang Shengxiao, mtafiti wa Chuo cha Chama cha Kamati Kuu ya CPC amesema, "Raundi mpya ya mapinduzi ya sayansi na teknolojia na mabadiliko makubwa ya viwanda imefungua mustakabali mpana kwa ajili ya kuendeleza nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora. Kutumia fursa hii ya kihistoria kunahitaji kuharakisha hatua za kufikia hali ya kujitegemea na kujiimarisha katika sayansi na teknolojia na kuongeza uwezo wa kufanya uvumbuzi katika mambo yote ili kudumisha utekelezaji wa hatua za kimkakati."
Mwongozo wa Mpango wa 15 wa Miaka Mitano (2026-2030) wa China unabainisha uendelezaji wa nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora kuwa jukumu muhimu la kimkakati, na umewekwa miradi mikubwa 28 inayohusiana na lengo hili, miradi ambayo inachukua asilimia 25.7 ya miradi yote mikubwa 109 iliyowekwa kwenye mpango huo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



