Lugha Nyingine
Wanawake wawili wa China watajwa miongoni mwa Wanawake 100 Mashujaa wa FAO

Wanawake wakifanya kazi ndani ya banda la kilimo cha kisasa cha kijani katika Mji Laoting wa Wilaya ya Laoting mkoani Hebei, kaskazini mwa China, Desemba 12, 2018. (Xinhua/Zhang Fengguo)
ROMA--Wanawake wawili wa China wametajwa miongoni mwa Wanawake 100 Mashujaa wa FAO chini ya Pendekezo la "Mifumo ya Kilimo-Chakula na Maendeleo ya Vijiji”, kwa mujibu wa orodha ya wanawake 99 waliotambuliwa ambayo ilitolewa hivi karibuni na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Wanawake hao wawili ni Yu Jinxiu, mtaalamu wa matibabu ya moxibustion kutoka Wilaya ya Qichun katika Mkoa wa Hubei katikati mwa China, na Dong Minfang, mkurugenzi wa Ushirika wa Kitaalamu wa Mashine za Kilimo wa Fengrui katika Wilaya ya Yueyang mkoani Hunan katikati mwa China.

Hii ni picha ya Yu Jinxiu, mtaalamu wa tiba ya moxibustion kutoka Wilaya ya Qichun katika Mkoa wa Hubei katikati mwa China, picha ambayo iliyotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Kwa kuadhimisha Mwaka wa Wakulima Wanawake wa Kimataifa wa 2026, Shirika la FAO limeanzisha kampeni ya dunia nzima ya kuwasifu wanawake 100 waliotoa mchango mkubwa katika kilimo, mifumo ya chakula na maendeleo ya vijiji.
Hafla ya utoaji tuzo itafanyika tarehe 15 Oktoba kwenye makao makuu ya FAO mjini Roma kama sehemu ya Jukwaa la Chakula Duniani la mwaka huu. Shirika la habari la China, Xinhua limefahamishwa kuwa mshindi mwingine atatangazwa kwenye hafla hiyo.
FAO imesema ilipokea mapendekezo 609 kutoka kwa nchi wanachama wake 131, na mchakato wa uteuzi ulihusisha uhakiki wa hali ya kustahiki, tathmini na upangaji wa nafasi za washindi uliofanywa na menejimenti ya waandamizi, pamoja na raundi mbili za majadiliano.
Kwa mujibu wa tovuti ya FAO, Yu ni mtaalamu anayeongoza katika matibabu ya Moxibustion ya Qichun, ambayo ni mali ya urithi wa utamaduni usioshikika unaotambulika kitaifa nchini China. Pia ni balozi wa chapa ya huduma ya kazi ya "Mtaalamu wa matibabu ya Moxibustion ya Qichun."
Katika miongo miwili iliyopita, Yu amewaandaa wataalamu zaidi ya 30,000 wa matibabu ya moxibustion na kuwasaidia maelfu ya watu kupata nafasi za ajira au kuanzisha shughuli zao wenyewe, na kuwasaidia wakazi wa vijijini kuongeza vipato, hasa wanawake na watu wenye ulemavu.Dong anaongoza Ushirika wa Kitaalamu wa Mpunga wa Runsheng na Ushirika wa Kitaalamu wa Mashine za Kilimo wa Fengrui katika Wilaya ya Yueyang.
Baada ya kuacha kazi yenye mafanikio katika sekta ya ushirika na kurejea kwenye kilimo katika eneo analotoka, ameongoza juhudi za kupanua uzalishaji wa nafaka kwa kutumia mashine na kuunga mkono wakulima wadogo. Pia amesaidia kuongeza nafasi za ajira, utoaji wa mafunzo na ujasiriamali kwa wanawake wa vijijini.
Umoja wa Mataifa uliutangaza mwaka 2026 kuwa Mwaka wa Wakulima Wanawake wa Kimataifa ili kuangazia mchango waliotoa wanawake katika mifumo ya kilimo na chakula, na kuhimiza kuboresha sera na uwekezaji vinavyoweza kuwasaidia wanawake kupata ufadhili, ujuzi na huduma.

Hii ni picha ya Dong Minfang, mkurugenzi wa Ushirika wa Kitaalamu wa Mitambo ya Kilimo wa Fengrui katika Wilaya ya Yueyang mkoani Hunan, katikati mwa China, iliyotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



