Lugha Nyingine
Teknolojia za kijani za China zahuisha kiwanda cha saruji nchini Afrika Kusini

Picha hii iliyopigwa tarehe 18 Agosti 2026 ikionesha kitengo cha kuzalisha umeme kwa kutumia joto la ziada kwenye Kiwanda cha Saruji cha Simuma katika Jimbo la KwaZulu-Natal, Afrika Kusini. (Xinhua/Chen Wei)
DURBAN, Afrika Kusini – Katika Jimbo la KwaZulu-Natal la Afrika Kusini, kiwanda cha saruji cha Simuma ambacho kimekuwa kikifanya kazi kwa zaidi ya miongo minne kinapata sura mpya.
Katika kiwanda hicho, ambacho kilinunuliwa na kampuni ya Nyenzo za Ujenzi ya Huaxin ya China mwezi Desemba 2023, mitambo ya zamani inaboreshwa, joto la ziada linabadilishwa kuwa umeme, na malori ya uchimbaji madini yanayotumia umeme yanakuwa mbadala wa yale yanayotumia dizeli. Wakati huo huo, wafanyakazi wenyeji wanapata ujuzi wa kiufundi kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu wa kivitendo na wenzao Wachina.
Kiwanda hicho cha Simuma awali kilikuwa kituo kikuu cha uzalishaji cha kampuni ya Simenti ya Natal Portland (NPC), moja ya kampuni kongwe za kuzalisha saruji nchini Afrika Kusini. Ingawa kiwanda hicho kilikuwa na mfumo imara wa uzalishaji na mtandao wa usambazaji, baadhi ya mitambo ilikuwa imefanya kazi kwa miongo kadhaa, jambo lililoongeza gharama za uzalishaji na kupunguza ufanisi na uwezo wa uzalishaji.
Baada ya kukinunua NPC, Huaxin ilikifanya kiwanda hicho cha Simuma kuwa eneo muhimu kwa ajili ya uboreshaji wa teknolojia na upanuzi wa uwezo.
"Shughuli hapa zilianza mwaka 1984, muda mrefu uliopita. Hivyo, kulikuwa na uhitaji mkubwa wa kuboreshwa, kufanywa kuwa cha kisasa na kuongezewa ufanisi," amesema Meneja wa Kiwanda cha Simuma, Rory Govender. "Tulifurahi sana wakati Huaxin ilipochukua uongozi wa kiwanda na kuanza upanuzi na uboreshaji. Ni jambo tulilolitaka kwa muda mrefu."
Badala ya kubadilisha mitambo yote ya kiwanda, Huaxin imejikita katika maboresho mahsusi, ikitumia miundombinu iliyopo wakati huohuo ikishughulikia changamoto kuu zinazokwamisha uzalishaji.
"Si tu tunachukua suluhu kutoka China na kuitumia hapa. Tunachunguza mitambo iliyopo na mazingira halisi nchini Afrika Kusini na kufanya maboresho mahsusi," amesema Wang Dongdong, meneja wa matengenezo wa kiwanda hicho.
Kwa mujibu wa Govender, uzalishaji wa kila siku wa clinker (malighafi ya saruji) kutoka kwenye Tanuri No.2 umeongezeka kutoka tani takriban 1,500 hadi tani 4,000, huku Tanuri No. 1, ambalo limekuwa likifanya kazi kwa miongo zaidi ya minne, likiongeza uzalishaji kutoka tani takriban 1,500 hadi tani 2,200 kwa siku.
Maboresho hayo ya mistari ya uzalishaji yameambatana na mabadiliko katika namna kiwanda hicho kinavyotumia nishati. Uzalishaji wa saruji ni mchakato wa viwandani unaohitaji kiasi kikubwa cha nishati na kuzalisha joto jingi. Katika kiwanda cha Simuma, joto la ziada ambalo lingepotea bure sasa linakusanywa na kubadilishwa kuwa nishati ya umeme.
Govender amesema kuwa mfumo huo wa kukusanya joto la ziada—ulioanzishwa kama sehemu ya jitihada za Huaxin za kuboresha ufanisi wa nishati na kupunguza uzalishaji wa gesi zinazosababisha ongezeko la joto duniani—umewezesha kiwanda hicho kuzalisha sehemu ya umeme wake wenyewe.
Mabadiliko hayo ya kijani yamefika pia katika machimbo ya mawe ya chokaa. Kampuni hiyo ya Huaxin imeanzisha matumizi ya malori makubwa ya uchimbaji yanayotumia umeme—yakitumia teknolojia mpya za nishati kutoka China—na hivyo kuchukua nafasi ya magari ya kawaida yanayotumia dizeli hatua kwa hatua.
Mabadiliko haya hayaonekani tu kwenye mitambo na takwimu za uzalishaji; yanabadilisha pia ujuzi na njia za maendeleo ya kikazi ya wafanyakazi wenyeji.
Kufuatia ununuzi huo, kampuni ya Huaxin ilidumisha muundo wa usimamizi wa wenyeji wa kiwanda hicho, wakati huohuo imeleta wataalamu wa kiufundi kutoka China kufanya kazi pamoja na timu za wenyeji katika upanuzi na uboreshaji wa kiwanda. Mwongozo katika eneo la kazi, mafunzo mahsusi kwa ajili ya majukumu husika, na mabadilishano ya kiufundi ya kila siku vimekuwa sehemu ya mchakato huo.
Eugene Bray, meneja wa mradi wa upanuzi wa kiwanda hicho, amesema kuwa mafunzo hayo yameimarisha uwezo wa kiufundi na kujiamini kwa wafanyakazi wenyeji.
Bray ameongeza kuwa mradi huo wa upanuzi na uboreshaji ulitengeneza ajira takriban 800 za muda, zikileta manufaa kwa jamii zinazoishi katika umbali wa kati ya kilomita tano hadi 50 kutoka kiwanda hicho.

Picha hii, iliyopigwa tarehe 18 Agosti 2026, ikionesha kiwanda cha saruji cha Simuma kilichopo katika Jimbo la KwaZulu-Natal, Afrika Kusini. (Xinhua/Chen Wei)

Meneja wa Kiwanda cha Simuma, Rory Govender, akizungumza kwenye mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua katika Jimbo la KwaZulu-Natal, Afrika Kusini, tarehe 18 Agosti 2026. (Xinhua/Chen Wei)

Lori la kubeba mizigo migodini linalotumia umeme likifanya kazi kwenye Kiwanda cha Saruji cha Simuma katika Jimbo la KwaZulu-Natal, Afrika Kusini, tarehe 18 Agosti 2026. (Xinhua/Chen Wei)

Wafanyakazi wakifuatilia uendeshaji wa vifaa ndani ya chumba kikuu cha udhibiti kwenye Kiwanda cha Saruji cha Simuma katika Jimbo la KwaZulu-Natal, Afrika Kusini, tarehe 18 Agosti 2026. (Xinhua/Chen Wei)

Picha hii iliyopigwa tarehe 4 Septemba 2025 ikionesha mnara wa kupasha joto awali (preheater tower) kwenye Kiwanda cha Saruji cha Simuma katika Jimbo la KwaZulu-Natal, Afrika Kusini. (Xinhua/Chen Wei)

Picha iliyopigwa tarehe 18 Agosti 2026 ikionesha mandhari ya Kiwanda cha Saruji cha Simuma katika Jimbo la KwaZulu-Natal, Afrika Kusini. (Xinhua/Chen Wei)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



