Lugha Nyingine
Wiki ya Nishati ya Afrika yafunguliwa Cape Town kutoa wito wa ushirikiano wa nishati barani Afrika

Wajumbe wakishiriki kwenye shughuli za Wiki ya Nishati ya Afrika (AEW) 2026 jijini Cape Town, Afrika Kusini, Oktoba 13, 2026. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)
CAPE TOWN - Wiki ya Nishati ya Afrika (AEW) 2026 imefunguliwa rasmi jijini Cape Town Jumanne wiki hii, huku Afrika Kusini ikitoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa nishati barani Afrika ili kuhakikisha utoaji wa nishati unakuwa vya kutosha na kwa bei nafuu, katika hali inayokabiliwa na mivutano ya siasa za kijiografia duniani na mivurugiko ya masoko.
Naibu Waziri wa Maliasili za Madini na Petroli wa Afrika Kusini, Phumzile Mgcina, ametoa wito huo kwenye hafla ya kufunguliwa kwa wiki hii ya nishati, akisema hali ya hivi sasa ya dunia nzima inaonesha kuwa ni lazima kujenga mfumo wa nishati wa Afrika ulio jumuishi na himilivu zaidi.
"Mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati umeonesha kwa mara nyingine namna hali katika eneo moja inavyoweza kuwa na athari kubwa kwa nchi na jamii zilizo umbali wa maelfu ya kilomita," amesema Mgcina. "Na hali hiyo inayoendelea imesababisha kupanda kwa bei za mafuta na gharama za maisha."
Amesema uhalisia huo wa mambo unawataka viongozi wa Afrika kuchukua hatua za uongozi thabiti, si kama tu kuimarisha viwanda vya nishati vya kila nchi ya Afrika bali pia kufanya juhudi kwa pamoja za kujenga mfumo wa nishati wa Afrika ulio wa jumuishi na uhimilivu ambao unaweza kujitosheleza.
Pia amesisitiza umuhimu wa kutegemea vyanzo mbalimbali vya utoaji wa nishati na kuimarisha biashara ndani ya bara hilo, akitoa mfano wa uzoefu wa Afrika Kusini wa kupata bidhaa za petroli kutoka masoko mbalimbali wakati huu ambapo kuna mivurugiko ya utoaji wa nishati wa kimataifa.
Amesema hakuna nchi yoyote ya Afrika inayoweza kufikia usalama wa nishati wa kudumu peke yake, kwani masoko, miundombinu, na maliasili vinahusiana, jambo ambalo linafanya ushirikiano wa kikanda kuwa muhimu zaidi.
Mgcina pia ametoa wito wa kuchukua mbinu yenye uwiano katika maendeleo ya nishati, na ameeleza kuwa nchi nyingi za Afrika bado zinakabiliwa na upungufu na uhaba wa nishati, uwezo mdogo wa viwanda, na miundombinu isiyo ya kutosha.
Wito huo wa Mgcina wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya nishati umeungwa mkono na Waziri wa Nishati na Petroli wa Senegal, El Hadji Abdourahmane Diouf, ambaye amesisitiza umuhimu kwa nchi za Afrika kuendeleza mifumo ya mafungamano ya nishati.
Diouf amesema kuwa Afrika inahitaji kuunda mfumo wake yenyewe wa maendeleo ya nishati na kuhakikisha nishati inaopatikana inaweza kuunga mkono ukuaji wa viwanda na kubadilisha muundo wa uchumi. "Afrika lazima ipewe fursa ya kuendeleza mfumo wake yenyewe wa nishati," amesema.
Wiki ya Nishati ya Afrika (AEW) ilifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2021, nayo ikiwa jukwaa la majadiliano juu ya uwekezaji katika nishati, ruhusa ya kuingia masoko na ukuaji wa viwanda, na ikiwafanya wadau wanaohusiana na maslahi ya pande mbalimbali wakusanyike pamoja ili kutoa matarajio ya pamoja juu ya mustakabali wa nishati wa Afrika.

Naibu Waziri wa Maliasili za Madini na Petroli wa Afrika Kusini, Phumzile Mgcina, akizungumza kwenye hafla ya kufunguliwa kwa Wiki ya Nishati ya Afrika (AEW) 2026 jijini Cape Town, Afrika Kusini, tarehe 13 Oktoba 2026. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)

Wajumbe wakishiriki kwenye hafla ya kufunguliwa kwa Wiki ya Nishati ya Afrika (AEW) 2026 jijini Cape Town, Afrika Kusini, tarehe 13 Oktoba 2026. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



