Botswana yatumia uchimbaji madini kama kichocheo cha mabadiliko makubwa ya kitaifa, uwezeshaji raia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 28, 2026

Mshiriki wa Maonesho ya Uchimbaji Madini ya Botswana akitembelea banda la mwoneshaji bidhaa kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Gaborone, Gaborone, Botswana, Oktoba 27, 2026. (Xinhua/Guo Chunju)

Mshiriki wa Maonesho ya Uchimbaji Madini ya Botswana akitembelea banda la mwoneshaji bidhaa kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Gaborone, Gaborone, Botswana, Oktoba 27, 2026. (Xinhua/Guo Chunju)

GABORONE - Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Ulinzi na Usalama wa Botswana Moeti Mohwasa amesema sekta ya uchimbaji madini ya Botswana lazima iwe kichocheo cha mabadiliko mapana zaidi ya kitaifa, ikienda zaidi ya uchimbaji wa madini hadi uwezeshaji wa watu.

Mohwasa ametoa kauli hiyo jana Jumanne wakati akitoa hotuba kuu chini ya mada "Uchimbaji Madini kwa Mabadiliko Makubwa ya Kitaifa: Kuimarisha Utawala, Kuufanya Uchumi Kutegemea Sekta Mbalimbali na Ustawi wa Raia," na kufungua rasmi Maonesho ya Uchimbaji Madini ya Botswana ya siku tatu kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Gaborone katika mji mkuu wa nchi hiyo.

"Lazima tuwekeze katika ukuzaji ujuzi, kuzipa jamii fursa zaidi za uchimbaji madini, kuufanya uchumi wetu kutegemea sekta mbalimbali, na kuboresha maisha ya wale wanaoishi katika maeneo ya uchimbaji madini," amesema.

"Utajiri wetu wa madini lazima ujidhihirishe katika fursa endelevu, ukuaji jumuishi, na ustawi wa kudumu kwa raia wetu," amebainisha. "Kipimo halisi cha utajiri wetu wa madini si tu kile tunachochimba kutoka ardhini, bali pia jinsi tunavyobadilisha kwa kiasi kikubwa maisha ya watu wetu."

"Awamu yetu inayofuata ya ukuaji haitapimwa tu kwa kile tunachochimba kutoka ardhini, bali pia kwa namna tunavyounganisha kwa ufanisi kile tunachochimba na masoko, viwanda, na watu wetu," amesema Letlhogonolo Barongwang, naibu waziri wa Wizara ya Uchukuzi na Miundombinu, kwenye shughuli hiyo.

Amesema serikali ya Botswana inalenga kuifanyia mabadiliko makubwa Botswana kutoka kuwa nchi isiyo na bandari hadi nchi iliyounganishwa na ardhi. Amesema miundombinu ya usafiri ni kiwezeshi cha maendeleo ya madini, uwezeshaji raia na biashara ya kikanda, huku usafiri bora ukiwa ni uti wa mgongo wa sekta ya madini yenye uwezo wa kushindana, kupunguza gharama kwenda sokoni, kuboresha usalama na kufungua thamani katika mnyororo mzima wa thamani ya madini.

Maonesho hayo ya Uchimbaji Madini ya Botswana 2026 yanawakutanisha viongozi wa sekta hiyo ili kufungua kizazi kijacho cha fursa za madini za Botswana kupitia mazungumzo ya kimkakati, maonesho, kujenga mitandao, na ushirikiano ambao unachochea utafutaji, uwekezaji, ukuaji endelevu, na kuufanya uchumi kutegemea sekta mbalimbali kote barani Afrika.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulika na Ulinzi na Usalama wa Botswana Moeti Mohwasa akizungumza kwenye ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Madini ya Botswana, Gaborone, Botswana, Oktoba 27, 2026. (Xinhua)

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulika na Ulinzi na Usalama wa Botswana Moeti Mohwasa akizungumza kwenye ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Madini ya Botswana, Gaborone, Botswana, Oktoba 27, 2026. (Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha