Lugha Nyingine
China yapanua ufikiaji wa biashara za kigeni kwenye bandari kubwa zaidi duniani ya biashara huria

Picha iliyopigwa Agosti 4, 2026 ikionesha watalii wakiwa wamepanda boti za utalii mjini Sanya, Mkoa wa Hainan, kusini mwa China. (Xinhua/Zhao Yingquan)
BEIJING - China imetangaza hatua 16 ili kurahisisha kampuni na wataalamu wa kigeni kufanya kazi kwenye Bandari ya Biashara Huria ya Hainan (FTP), ambayo ni bandari kubwa zaidi duniani ya biashara huria kwa ukubwa wa eneo, huku sera hizo mpya zilizotangazwa zikihusu biashara ya nishati, huduma za matibabu na shughuli za biashara zenye dhamana ya kikodi, kwa mujibu wa waraka wa serikali uliotolewa kwa umma jana Alhamisi.
Kwa mujibu wa hatua hizo, madaktari wa kigeni walio na leseni halali ya kufanya kazi ya udaktari nje ya nchi wanaweza kupata vibali vya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu kisiwani Hainan kwa hadi miaka mitatu, huku vibali hivyo vikiweza kuongezwa muda wake kwa mujibu wa kanuni husika.
Sera rahisi zaidi kuhusu vibali vya kazi na kukaa na kuishi pia zitaanzishwa kwa raia wa kigeni.
Bandari ya Biashara Huria ya Hainan, iliyoko katika mkoa wa kisiwa ulio kusini kabisa mwa China, ilizindua uendeshaji maalum wa forodha kisiwani kote mwezi Desemba 2025, ikiruhusu kuingia kwa bidhaa za nje kwa uhuru zaidi, kupanua wigo wa bidhaa zinazostahiki kwa ushuru-sifuri na kutekeleza hatua nyingine zinazorahisisha biashara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za China za kuhimiza ufunguaji mlango wa kiwango cha juu.
Kampuni za nje ya China zitaruhusiwa kutumia vifaa vyenye dhamana ya kikodi katika vituo vya kupokea gesi asilia ya kimiminika (LNG) vya Hainan, huku bandari hiyo ya Biashara Huria ikiwezesha kufanya uendeshaji wa shughuli za ghala la kukabidhi gesi asilia ya kimiminika (LNG) kwa wateja kwa mikataba ya hatima ya LNG inayozingatia hali za baadaye kuanza kufanya kazi.
Hatua zingine ni pamoja na kuhimiza biashara ya nje ya nchi, kupanua aina za bidhaa zinazostahiki kwa matengenezo ya dhamana ya kikodi, kuwezesha kuingia kwa bidhaa stahiki zenye dhamana ya kikodi zilizotengenezwa upya kwenye maeneo ya majaribio ya biashara huria katika China Bara, kuhamasisha matumizi ya yuan katika aina mpya za biashara ya kubadilishana bidhaa, na kuzidisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa bandari hiyo ya Biashara Huria na Mkoa wa Utawala Maalum wa Hong Kong wa China.
Idadi ya kampuni mpya zenye uwekezaji wa kigeni kisiwani Hainan iliongezeka kwa asilimia 38.6 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia katika nusu ya kwanza ya 2026, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Serikali ya China ya Usimamizi wa Soko.
China imetangaza mipango ya kupanua zaidi wigo wa ufunguaji mlango kwa majaribio katika sekta kama vile huduma za mawasiliano ya simu zenye thamani iliyoongezwa, bioteknolojia na hospitali zinazomilikiwa na wageni pekee, wakati huohuo ikichukua hatua kuwezesha biashara na uwekezaji wa kuvuka mipaka.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



