Lugha Nyingine
Maafisa wa Botswana na China waahidi ushirikiano wa karibu zaidi

Wasanii wa Botswana wakicheza ngoma ya asili kwenye shughuli ya "Jioni ya Urafiki kati ya Botswana na China" iliyofanyika Gaborone, Botswana, tarehe 31 Oktoba 2026. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)
GABORONE - Maafisa kutoka Botswana na China wameahidi kuimarisha urafiki na kuzidisha ushirikiano ili kubadili maoni muhimu ya pamoja yaliyofikiwa na viongozi wa nchi hizo mbili kuwa manufaa halisi kwa watu wa pande zote mbili kwenye hafla ya "Jioni ya Urafiki kati ya Botswana na China" iliyofanyika Gaborone, Botswana.
Akitoa hotuba kuu kwenye hafla hiyo iliyofanyika Jumamosi kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Gaborone, katika mji mkuu, Rais Duma Boko wa Botswana ameielezea ziara yake ya hivi karibuni ya kitaifa nchini China kuwa "yenye mafanikio kupita matarajio."
Matokeo ya ziara hiyo yatabadilishwa kuwa "fursa na manufaa halisi kwa watu wetu," amesema Boko, huku akiihimiza Botswana kujifunza kutokana kwenye uzoefu wa maendeleo wa China katika nyanja za ujuzi, utaalamu, uvumbuzi, na teknolojia.
Ameipongeza sera ya China ya ushuru-sifuri kwa nchi za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China, akisema kuwa inafungua soko kubwa la China kwa bidhaa za Afrika. Ameongeza kuwa Botswana inahitaji kuongeza uzalishaji na kuboresha kiasi na ubora wa bidhaa zake.
Boko amesema Botswana inakaribisha wawekezaji wa China ili kuchangia uzoefu wao kwa ajili ya uhamishaji ujuzi. Amesisitiza nafasi ya kimkakati kijiografia ya nchi hiyo ya katikati mwa Kusini mwa Afrika, akiielezea kuwa ni lango la mtiririko wa mitaji kuingia barani humo.
Balozi wa China nchini Botswana, Fan Yong, amesema kuwa China iko tayari kufanya kazi na pande zote za Botswana ili kutekeleza kikamilifu maoni muhimu ya pamoja yaliyofikiwa na viongozi wa nchi hizo mbili, kuimarisha ushirikiano katika sekta za uchumi wa kidijitali, kilimo, ufugaji, huduma ya afya, na elimu, ili kuunga mkono maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Botswana.
Shughuli hiyo ya "Jioni ya Urafiki kati ya Botswana na China" iliandaliwa kwa pamoja na Jumuiya ya Urafiki kati ya Botswana na China, Jumuiya ya Wasanii wa Quyi, China, na shirika la Business Botswana, kwa uungaji mkono kutoka Wizara ya Michezo na Sanaa ya Botswana na Ubalozi wa China nchini Botswana.
Shughuli hiyo ilijumuisha kipindi cha utamaduni na sanaa, ikiwemo utamkaji wa maneno magumu, sanaa ya “kubadilisha sura” kutoka Opera ya Sichuan, na maonesho ya vichekesho vya kutumia ishara (mime) ya wasanii wa China vilevile ushairi wa asili, ngoma, na maonesho ya ala ya 'Setinkane' kutoka kwa wasanii wa Botswana.
Uzinduzi wa hafla ya Tuzo ya Urafiki ya Almasi kati ya Botswana na China, pia ulifanyika kwenye shughuli hiyo.

Rais wa Botswana Duma Boko akitoa hotuba kuu kwenye shughuli ya "Jioni ya Urafiki kati ya Botswana na China" iliyofanyika Gaborone, Botswana, tarehe 31 Oktoba 2026. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

Msanii Mchina akifanya onesho la “kubadilisha sura” kutoka Opera ya Sichuan kwenye shughuli ya "Jioni ya Urafiki kati ya Botswana na China" iliyofanyika Gaborone, Botswana, tarehe 31 Oktoba 2026. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



