Lugha Nyingine
Maonesho ya 9 ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China yaanza mjini Shanghai; mambo matano yaipa nafasi Afrika
Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China (CIIE) yamefunguliwa rasmi Alhamisi kwenye Kituo cha Kitaifa cha Maonesho na Mikutano (Shanghai) mjini Shanghai, Mashariki mwa China.
Maonesho haya ambayo yanaandaliwa na Wizara ya Biashara ya China na Serikali ya Mji wa Shanghai na kuratibiwa maandalizi yake na Ofisi ya Maonesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China yamepangwa kufanyika kuanzia Novemba 5 hadi 10 yakiwa na kaulimbiu ya “Zama Mpya, Mustakabali wa Pamoja”.
Kwa mujibu wa waandaaji wa maonesho haya, ushiriki mwaka huu umekuwa wa aina yake. Jumla ya nchi na maeneo 162 yakiwemo mashirika ya kimataifa yanashiriki sambamba na kampuni 4,142 za kigeni. Idadi ya kampuni kutoka Kampuni Bora 500 duniani (Fortune Global 500) na viongozi wa mambo ya viwanda imezidi 300 kwa mara ya kwanza. Aidha, ukubwa wa eneo la maonesho umezidi mita za mraba 440,000 kwa mara ya kwanza pia.
Maonesho haya, yanajumuisha kumbi mbalimbali zenye kuonesha mambo kama vile magari, vifaa tiba na bidhaa za huduma za afya, AI na teknolojia ya kupashana habari, bidhaa za wanunuzi, bidhaa za chakula na kilimo, na biashara katika huduma.
Kila mwaka kwenye maonesho haya, waandaaji kipekee wamekuwa wakitoa jukwaa pana zaidi na uwezeshaji kwa bidhaa na wafanyabiashara wa Afrika ili kulifikia soko kubwa la China na kukutana ana kwa ana na wanunuzi na wafanyabiashara wa China na kwingineko. Kwenye maonesho ya mwaka huu kuna mambo ya kipekee na mahsusi matano kuhusu Afrika ambayo ni ya kuangaliwa kwa karibu na yenye kuipa nafasi zaidi.
Kwanza; maonesho haya ni ya kwanza tangu China itangaze kuanza kutekeleza sera ya kutoza ushuru-sifuri kwa nchi za Afrika ambazo ina uhusiano wa kidiplomasia nazo mapema Mei Mosi mwaka huu. Kwa maana hiyo, maonesho haya yanatoa fursa kwa nchi za Afrika, kunufaika hasa na sera hii ambapo waoneshaji bidhaa wa Afrika wanalifikia soko la China moja kwa moja huku wakiingiza bidhaa mpya zilizoongezwa thamani na kuzitambulisha bila kulipia ushuru.
Pili; waandaaji wa maonesho haya wameandaa Eneo Maalum la Bidhaa za Afrika na Asia kwa mara ya kwanza. Kupitia eneo hili wanunuzi na wafanyabiashara wa ndani na nje ya China wanapata fursa kupata taarifa zote katika eneo moja, ikiwawezesha kuwasiliana na wajasiriamali na waoneshaji bidhaa wa Afrika kwa urahisi na hivyo kuongeza mwonekano na usambazaji wa bidhaa zao duniani.
Tatu; kwa mujibu wa waandaaji, nchi za Gabon na Côte d'Ivoire zinashiriki kwa mara ya kwanza na mabanda ya kitaifa kwenye maonesho haya, na kufanya idadi ya nchi za Afrika kwenye maonesho haya kufikia karibu nchi zote zenye uhusiano wa kidiplomasia na China.
Kwa uzito wa ushiriki wa Gabon, Rais wa Gabon Brice Clotaire Oligui Nguema ni miongoni mwa wageni mashuhuri walioshiriki hafla ya kufungua maonesho haya ya mwaka huu.
Nne; kwa mujibu wa machapisho ya waandaaji wa maonesho haya, kuna usaidizi mahsusi unaotolewa kwa waoneshaji bidhaa wa nchi za Afrika ambao wanakidhi mahitaji na vigezo kadhaa. Usaidizi huo unahusu kuwapa mabanda kwa bei nafuu au bure, kuwezesha bidhaa zao kuidhinishwa kupitia njia ya haraka, kutoa ruzuku kwenye gharama za kusafirisha kuleta bidhaa na kadhalika.
Na tano; waandaaji wamepanga shughuli za kukutanisha waoneshaji bidhaa wa Afrika na wanunuzi lakini pia kuwezesha wafanyabiashara wa Afrika kujenga mitandao ya biashara na wenzao wa China na duniani. Miongoni mwa shughuli zilizopangwa na waandaaji ni pamoja na zile za kunadi uwekezaji, ujengaji mitandao ya biashara na kukutanisha wauzaji bidhaa na wanunuzi.
Ukiongeza na Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la Hongqiao ambalo mwaka huu linafanyika chini ya kaulimbiu ya “Utulivu na Ushirikiano: Kujenga Uchumi Wazi Pamoja”, maonesho haya si tu ni fursa ya kipekee kwa Afrika kuonesha bidhaa na mazao yake maalum kwa dunia lakini pia ni jukwaa pana zaidi la kuhimiza uchumi ulio wazi, wenye manufaa na jumuishi kwa wote. Ni nyenzo muhimu ya kuchochea ushirikiano miongoni mwa wadau katika kujenga uchumi himilivu wa dunia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




