Lugha Nyingine
Tanzania yaja kwenye CIIE na taasisi muhimu, yalenga uwekezaji, kukuza mauzo ya nje (2)
SHANGHAI, China – Tanzania imetumia Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China (CIIE) kuimarisha juhudi za kupanua mauzo ya nje, kuvutia wawekezaji na kufungua fursa mpya za kibiashara, kupitia ushiriki wa taasisi zake muhimu za Serikali.
Taasisi hizo ni Bodi ya Chai Tanzania, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maaulum ya Kiuchumi (TISEZA), ambazo zimekuja kuunganisha wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania na wanunuzi pamoja na wawekezaji wa China.
Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania, Beatrice Banzi, akizungumza katika mahojiano maalum na People's Daily Online kwenye Banda la Tanzania la maonesho hayo Jumamosi, Novemba 7 amesema ushiriki wao unalenga kupanua soko la chai ya Tanzania nchini China, kuimarisha masoko yaliyopo na kuitangaza bidhaa hiyo kimataifa.
Amesema China ni miongoni mwa masoko muhimu ya chai duniani, hivyo CIIE inatoa fursa kwa Tanzania kuongeza mauzo na kujenga ushirikiano mpya wa kibiashara.
“Kuitangaza chai ya Tanzania hapa ni kuitangaza duniani kwa nchi nyingi kwa wakati mmoja, kwa sababu zinashiriki zaidi ya nchi 100 kwenye jukwaa moja,” amesema Banzi.
Ameeleza kuwa mauzo ya chai ya Tanzania nchini China yamekuwa yakiongezeka tangu mwaka 2023, huku ukuaji ukiimarika zaidi mwaka 2025 na 2026 kutokana na sera rafiki za kodi, hususan sera ya ushuru-sifuri.
Ameongeza kuwa tayari kampuni mbili za China zimeonesha nia ya kuagiza chai kutoka Tanzania kwenye maonesho hayo, zikiomba sampuli na mawasiliano kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa kibiashara.
Kwa upande wake, Afisa Biashara wa TanTrade, Feliciana Samwel Mbaga, amesema taasisi hiyo inaratibu ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya ndani na nje ya nchi kwa lengo la kutangaza bidhaa za Tanzania na kuimarisha utambulisho wa chapa ya Made in Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Amesema CIIE ni jukwaa muhimu la kuwaunganisha wazalishaji wa ndani na wanunuzi wa kimataifa, akibainisha kuwa idadi ya waoneshaji wa Tanzania mwaka huu imeongezeka maradufu kutoka takribani tisa mwaka uliopita.
Naye Afisa Uhusiano wa WRRB, Augusta Njoji, amesema bodi hiyo inalenga kuwaunganisha wanunuzi wa China na wafanyabiashara wa Tanzania kwa kuwapatia taarifa sahihi kuhusu kiasi, viwango na ubora wa mazao yanayohifadhiwa kwenye maghala.
“Kazi yetu ni kumhakikishia mnunuzi kuhusu ubora wa mazao, kuanzia kushiriki kwenye minada, kuchagua na kununua hadi kuyachukua na kuyasafirisha nje ya nchi yakiwa katika ubora na viwango anavyohitaji,” amesema Njoji.
Ameongeza kuwa kupitia CIIE, WRRB inalenga kujenga mitandao ya kibiashara itakayowezesha wanunuzi na kampuni za China kushiriki katika minada ya mazao ya Tanzania ambayo tayari yamehakikiwa ubora na kupewa stakabadhi zake.
Wakati huohuo, BRELA inashiriki kwa mara ya kwanza katika maonesho hayo, ikilenga kuvutia kampuni za China kuwekeza Tanzania na kuzifahamu huduma za usajili wa biashara zinazopatikana nchini humo.
Aidha, Afisa Leseni wa BRELA, Robert Mashika, amesema wakala huo unataka kuwaunganisha wawekezaji wa China moja kwa moja na mifumo rasmi ya biashara ya Tanzania, kupunguza utegemezi wa mawakala na kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi.
“BRELA ni lango la biashara la Tanzania kwa sababu ndiyo inayosajili kampuni na wadau wanaotaka kufanya biashara au uwekezaji nchini. Tumekuja kuwaunganisha wawekezaji wa China moja kwa moja na huduma zetu,” amesema Mashika.
Amesema wafanyabiashara wa China wanaweza kukamilisha taratibu za usajili wa biashara au kampuni kwa njia ya mtandao wakiwa nchini mwao, bila kulazimika kusafiri hadi Tanzania kwa ajili ya hatua hizo pekee.
Ameeleza kuwa hatua hiyo itawasaidia wawekezaji kuokoa muda na gharama, ili wanapowasili Tanzania waweze kuelekeza nguvu zaidi katika kuanzisha ofisi na kuanza shughuli za biashara.
Cathy Wang, Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara na Lojistiki cha Afrika Mashariki (EACLC), ambao ni waratibu na wawezeshaji wa ushiriki wa Tanzania kwenye maonesho hayo kwa kushirikiana na Ubalozi wa China nchini Tanzania na serikali ya Tanzania, amesema ikilinganishwa na miaka iliyopita Tanzania imekuwa na ushiriki mkubwa.
“Maonesho ya nyuma, ilikuwa changamoto kupata washiriki, mwamko na uelewa ulikuwa mdogo. Mwaka 2021 tulipokuja kwa mara ya kwanza tulikuja na waoneshaji wachache sana na sampuli za kampuni sita tu. Lakini mwaka huu idadi imefika 36, unaweza kuona ongezeko kubwa” amesema Cathy.
Amesema, CIIE ni jukwaa muhimu kwanza katika kusaidia bidhaa na wafanyabiashara wa Tanzania kulifikia soko kubwa la China, pili; pia inasaidia kuwezesha bidhaa za Tanzania kufikia viwango vya ufungashaji na ubora wa kimtaifa, na tatu; ni fursa kwa Tanzania kufahamu na kutumia vema sera ya ushuru-sifuri ya China kwa nchi za Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




