Lugha Nyingine
Waziri wa Biashara wa Angola: Angola inatafuta kugeuza sera ya ushuru-sifuri ya China kuwa matokeo halisi katika CIIE (2)
SHANGHAI — Waziri wa Viwanda na Biashara wa Angola, Rui Miguêns de Oliveira amesema Angola inalenga kugeuza sera ya China ya ushuru-sifuri wa forodha kwa bidhaa kutoka nchi za Afrika kuwa fursa halisi za kibiashara, huku ushiriki wake katika Maonesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China (CIIE) ukidhihirisha azma yake hiyo kwa kunuwia kuongeza mauzo ya bidhaa zake kwenye moja ya masoko makubwa zaidi ya wanunuzi duniani.
Waziri huyo amesema maonesho hayo yanatoa jukwaa muhimu kwa wafanyabiashara wa Angola kuonesha bidhaa zao, kujenga uhusiano wa kibiashara na kutafuta fursa za kuingia katika soko la China.
Akizungumza katika mahojiano na People’s Daily Online Jumamosi Novemba 7 kwenye banda la nchi yake la maonesho hayo mjini Shanghai, waziri huyo ameeleza kufurahishwa na fursa ya kuwasilisha uwezo wa Angola katika uzalishaji wa bidhaa zinazoweza kuuzwa nje kwa wafanyabiashara na wanunuzi wa China na duniani, akieleza kuwa China ni soko muhimu kwa nchi zinazotaka kupanua biashara yake ya kimataifa.
“Tunashukuru sana kwa kupata fursa ya kuwasilisha uwezo wetu na bidhaa mbalimbali tulizonazo kwa ajili ya kuuza katika soko la China,” amesema.
Kwake yeye Angola, kushiriki katika maonesho hayo si suala la kuonesha bidhaa pekee, bali pia ni fursa ya kujenga uhusiano wa kudumu wa kibiashara na waagizaji bidhaa kutoka China na kujipatia nafasi katika soko hilo lenye ukubwa mkubwa na fursa nyingi kwa wasambazaji wa kimataifa.
Waziri huyo amekaribisha pia sera ya China ya ushuru-sifuri wa forodha kwa bidhaa kutoka nchi za Afrika, akiieleza kuwa ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara wa Afrika kuimarisha uwepo wao katika soko la China.
Amesema upatikanaji wa soko la China kwa masharti hayo ya upendeleo unaweza kuhamasisha wafanyabiashara wa Afrika kujenga uhusiano wa moja kwa moja na waagizaji bidhaa wa China, hatua itakayowawezesha kutafuta fursa mpya za kibiashara na kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao nje ya nchi.
“Ni jambo muhimu sana, hasa kwetu sisi Waafrika, kwa sababu ni njia mojawapo ya kuwawezesha wafanyabiashara wetu kutumia fursa hii kuanza kufanya biashara na waagizaji bidhaa kutoka China na kujipatia nafasi katika soko kubwa ambalo China inatoa,” amesema.
Waziri huyo amesema kampuni za Angola zinazoshiriki katika maonesho ya mwaka huu zimeazimia kutumia ipasavyo fursa zinazotolewa na mpango huo wa serikali ya China wa kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa za Afrika.
“Tunafurahia sana fursa hii, na tunaamini kuwa kampuni za Angola zimekuja hapa mwaka huu kufanya kila liwezekanalo ili kutekeleza kwa vitendo fursa zinazotolewa kupitia sera hii ya serikali ya China ya ushuru-sifuri,” amesema.
CIIE, ambayo ni miongoni mwa majukwaa makubwa ya China ya kukuza biashara na uwekezaji wa kimataifa, inazipa nchi zinazoshiriki fursa ya kuwaunganisha wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa na wanunuzi watarajiwa, pamoja na kutafuta njia za kuingia katika soko la China. Kwa mwaka huu maonesho hayo yalifunguliwa Novemba 5 na yamepangwa kufikia tamati Novemba 10.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




