Lugha Nyingine
Maonesho ya picha ya China na Afrika yazidisha urafiki na uhusiano wa kiutamaduni (2)
ADDIS ABABA - Maonesho ya Picha ya Taswira za China na Afrika yamefunguliwa jana Alhamisi mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, yakionesha uhusiano wa kiutamaduni, ubadilishanaji wa kati ya watu, na urafiki unaothaminiwa kwa muda mrefu kati ya China na Afrika.
Maonesho hayo, yanayofanyika kwenye Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika (UNECA), yanajumuisha picha 64 zilizochaguliwa kutoka kazi 283 zilizowasilishwa na wapiga picha 151 kutoka nchi 26.
Picha hizo zilipigwa katika nchi zaidi ya 30 za Afrika na China. Kati ya hizo, picha 24 zilishinda tuzo kwa kuonesha kwa namna ya kipekee uanuai wa China na Afrika, zikionesha maendeleo, mafanikio, urithi tajiri wa utamaduni, wanyamapori, na mandhari yao.
Akifungua maonesho hayo, Jiang Feng, Mkuu wa Ujumbe wa China katika Umoja wa Afrika, amesema maonesho hayo ni mfano dhahiri wa juhudi za pamoja za China na Afrika katika kutekeleza Pendekezo la Ustaarabu Duniani ambalo linatoa wito wa kuheshimu utofauti wa ustaarabu, ubadilishanaji imara zaidi wa kati ya watu ya kimataifa, na kuishi pamoja kwa mapatano na kufunzana.
"Maonesho haya yanatoa fursa ya kuzidisha zaidi kuelewana na urafiki kati ya watu wa China na Afrika, kuwezesha mabadilishano miongoni mwa ustaarabu ili kuvuka vizuizi, na kuwaleta watu wetu karibu zaidi kuvuka milima na bahari, hivyo kujenga msingi imara zaidi na wa kudumu zaidi wa uungaji mkono wa umma kwa urafiki kati ya China na Afrika," amesema Jiang.
Akibainisha kuwa urafiki kati ya China na Afrika una historia ndefu na umeendelea kuimarika kadiri muda unavyopita, Jiang ameeleza matumaini yake kuwa maonesho hayo yatafungua fursa mpya za kuongeza kuelewana kati ya watu wa China na Afrika, kuzidisha mabadilishano yao ya kitamaduni, na kusaidia kujenga jumuiya ya hali zote ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja.
Mama Keita, Naibu Katibu Mtendaji anayeshughulikia uungaji mkono wa programu katika UNECA, amesema picha hizo zinaonesha matukio ya maisha ya kila siku, zikileta pamoja maeneo, tamaduni, na mitazamo tofauti katika mazungumzo ya kuona, na kuheshimu vyote sifa za kipekee na ubinadamu wa pamoja.
"Natumai picha hizi zitachochea mazungumzo, kupanua mitazamo yetu, na kutuhimiza kutazama tamaduni, uzoefu, na urithi wetu mbalimbali kwa mtazamo mpya, huku tukigundua mambo ya pamoja ambayo yanaunganisha China na Afrika," amesema.
Maonesho hayo, yaliyoandaliwa kwa pamoja na Ujumbe wa China katika Umoja wa Afrika na UNECA, yamevutia wageni karibu 200. Pia, yanafanyika wakati pande hizo mbili zikiadhimisha Mwaka wa Mabadilishano ya Kati ya Watu wa China na Afrika.
"Tunapoadhimisha Mwaka wa Mawasiliano Kati ya Watu wa China na Afrika, tunakumbushwa kuwa uhusiano kati ya nchi haujengwi tu kupitia mikutano na mikataba, bali pia kupitia watu, shauku, uzoefu wa pamoja, ubadilishanaji wa kitamaduni, na simulizi tunazoelezeana," amesema Wubshet Tolosa, mwakilishi wa wapiga picha waliopokea tuzo, kwenye maonesho hayo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




