Iran yawasilisha rasimu ya mapendekezo kuhusu kuondolewa kwa vikwazo na udhibiti wa nyuklia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 03, 2021
Iran yawasilisha rasimu ya mapendekezo kuhusu kuondolewa kwa vikwazo na udhibiti wa nyuklia
Ali Bagheri Kani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Mpatanishi Mkuu wa nyuklia, akiwasili kwenye ukumbi wa mazungumzo ya makubaliano ya nyuklia ya Iran huko Vienna, Austria, Nov 29, 2021. (Xinhua/Guo Chen)

TEHRAN - Mpatanishi Mkuu wa Iran katika mazungumzo ya Vienna ametangaza Alhamisi ya wiki hii kwamba rasimu mbili za mapendekezo ya Iran juu ya kuondolewa vikwazo dhidi yake na udhibiti wa nyuklia zimewasilishwa kwa pande husika za makubaliano ya nyuklia ya Mwaka 2015, yanayojulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

"Kimantiki, upande mwingine unapaswa kusoma nyaraka hizi ili kujitayarisha kuzungumza na Iran kuhusu maandishi hayo," Ali Bagheri Kani ameviambia vyombo vya habari vya Iran katika Mji Mkuu wa Austria, Vienna.

Ameeleza matumaini yake kuwa pande husika za JCPOA zitaweza kupitia rasimu za Iran na kufikia hitimisho kuhusu nyaraka hizo "katika muda mfupi iwezekanavyo."

Bagheri pia alionya juu ya juhudi za pande zisizo kuwa sehemu ya makubaliano ya JCPOA kuvuruga kazi ya sasa ya kidiplomasia ili kufufua mpango huo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, mapema siku hiyo, Waziri Mkuu Naftali Bennett katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, alihimiza "kusitishwa mara moja kwa mazungumzo" na Iran na kutaka "utekelezaji wa hatua kali za nchi zenye ushawishi duniani" dhidi ya Iran.

Vyombo vya habari vya Israel viliripoti mapema wiki hii kuwa Serikali ya Israel imekuwa ikiwasiliana na maafisa wa Marekani na Ulaya katika muda wa wiki mbili zilizopita na kutoa upelelezi kuwa Iran imeendelea kuchukua hatua za kusafisha madini ya uranium kuwa kiwango cha silaha za nyuklia.

Hata hivyo siku ya Jumatano wiki hii Rafael Grossi, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) alikanusha madai hayo ya Iran kusafisha uranium kwa kiwango cha asilimia 90 na kubainisha kuwa IAEA ndiyo taasisi pekee ya inayosimamia vifaa vya nyuklia vya Iran.

Duru ya sasa ya mazungumzo ya JCPOA imeanza tena wiki hii mjini Vienna baada ya kusitishwa kwa takriban miezi sita, ikiwa ni takriban miezi mitatu tangu Serikali ya sasa ya Iran ichukue madaraka mwishoni mwa Mwezi Agosti mwaka huu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha