Afrika Kusini yafuatilia soko la China kwa uuzaji nje wa pombe kali za Brandy

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 07, 2021
Afrika Kusini yafuatilia soko la China kwa uuzaji nje wa pombe kali za Brandy
Mhudumu wa baa akihudumia kinywaji wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo kwenye shindano la pombe kali za brandy, yaani Brandy Innovation Challenge, mjini Cape Town, Afrika Kusini, Tarehe 6 Desemba 2021. Afisa mkuu wa kilimo katika Jimbo la Western Cape, nchini Afrika Kusini, eneo kuu la nchi hiyo kwa kuzalisha pombe kali, amesema jimbo hilo linatarajia masoko mapya nchini China kwa bidhaa zake zenye "kiwango cha kimataifa". (Xinhua/Lyu Tianran)

CAPE TOWN - Afisa wa juu wa Kilimo wa Jimbo la Western Cape nchini Afrika Kusini, ambalo ni eneo kuu la uzalishaji wa pombe kali za brandy nchini humo, amesema jimbo hilo linatarajia masoko mapya nchini China kwa ajili ya kuuza pombe kali zake aina ya brandy zenye "kiwango cha kimataifa".

Waziri wa Kilimo wa Jimbo hilo Ivan Meyer, ambaye pia ni Kiongozi wa shughuli za serikali wa jimbo hilo ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba, China ina idadi kubwa ya watu, na watu wengi wa China wanapenda pombe kali, ikiwa ni pamoja na brandy.

Amesema Jimbo la Western Cape limeanzisha uhusiano na China katika ngazi ya mkoa huku biashara ya nje na China ina historia ndefu.

“Tuko tayari kuingia katika soko la China,” amenukuliwa ofisa huyo.

Meyer pia amesema jimbo hilo, ambalo linachangia asilimia 53 ya mauzo ya nje ya kilimo nchini Afrika Kusini, tayari limesafirisha zabibu, matunda ya machungwa na mazao mengine ya kilimo kwenda China, na amebainisha kwamba China ina majukumu "muhimu sana" katika nyanja ya kilimo katika kufufua uchumi wa Western Cape kufuatia athari za UVIKO-19.

Shindano la pombe kali za Brandy, Brandy Innovation Challenge, lilitoa wito kwa wapenda uchanganyaji wa pombe kali za brandy kuunda chapa zao wenyewe na mpango wa biashara ili kusaidia ufufukaji wa uchumi. Washiriki watatu bora katika shindano hilo walipokea pesa za zawadi na watafundishwa na wafanyabiashara wakubwa wa pombe kali za Brandy ili kuanzisha biashara zao.

Hafla hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Pombe Kali za Brandy ya Afrika Kusini kwa ushirikiano na Waziri Mkuu wa Cape Magharibi Alan Winde na ilifanyika katika makazi yake rasmi.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, Pombe kali za brandy za Afrika Kusini zinakubalika kuwa mojawapo ya bidhaa bora zaidi duniani. Ilishinda mara 15 taji la Pombe Kali Bora Duniani katika Shindano la Kimataifa la Mvinyo na Pombe kali katika miaka 20 iliyopita.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha