Baraza la Usalama la UN lakutana kushughulikia ukosefu wa usalama wa chakula, latoa wito wa ushirikiano wa kimataifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 20, 2022

UMOJA WA MATAIFA - Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana Alhamisi wiki hii kwa lengo la kushughulikia tatizo la ukosefu wa usalama wa chakula na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuimarisha ushirikiano ili kulitatua.

"Vita vinapoanzishwa, watu huwa na njaa," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameliambia Baraza la Usalama wakati wa mjadala kuhusu migogoro na usalama wa chakula ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.

Guterres amesema, asilimia 60 ya watu wasio na lishe bora duniani wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro. "hakuna nchi iliyo salama." amesema.

Mwaka jana, wengi kati ya watu milioni 140 wanaokabiliwa na njaa kali duniani kote waliishi katika nchi 10 tu: Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Haiti, Nigeria, Pakistani, Sudan Kusini, Sudan, Syria na Yemen - nane kati ya hizo zipo kwenye ajenda za baraza hilo.

"Bila shaka: wakati baraza hili linajadili mgogoro, linajadili njaa. Unapofanya maamuzi kuhusu kulinda amani na misheni za kisiasa, unafanya maamuzi kuhusu njaa. Na unaposhindwa kufikia muafaka, watu wenye njaa hulipa gharama kubwa," Guterres amesema.

Licha ya kuwa na furaha kutangaza kwamba Mfuko Mkuu wa Kukabiliana na Dharura unatoa dola milioni 30 za Marekani ili kukidhi mahitaji ya usalama wa chakula nchini Niger, Mali, Chad na Burkina Faso, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kwa masikitiko: "Lakini hili ni tone kwenye bahari."

Guterres alielezea wasiwasi wake juu ya uhaba wa chakula katika eneo la Pembe ya Afrika, ambalo linakabiliwa na ukame mbaya zaidi katika miongo minne iliyopita, na kuathiri zaidi ya watu milioni 18, wakati nchini Ethiopia na Somalia, migogoro na ukosefu wa usalama unaendelea kuwakumba watu.

"Vita vya Ukraine sasa vinaongeza mwelekeo mpya wa kutisha kwenye hali hii ya njaa duniani," amesema Guterres huku akitoa mapendekezo manne kutatua hali ya ukosefu wa usalama wa chakula.

"Muhimu zaidi ya yote, tunahitaji kumaliza vita nchini Ukraine," amesema, akitoa wito kwa Baraza la Usalama kufanya kila liwezekanalo "kunyamazisha bunduki na kuhimiza amani, nchini Ukraine na sehemu mbalimbali duniani."

Pili, amesisitiza umuhimu wa kulinda ufikiaji wa kibinadamu na bidhaa na vifaa muhimu kwa raia, akitoa tahadhari ya "jukumu muhimu kwa nchi wanachama la kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu, na kutaka uwajibikaji pale zinapokiukwa."

Tatu, amesema kunahitajika "uratibu na uongozi mkubwa zaidi" ili kupunguza hatari zilizounganishwa za ukosefu wa usalama wa chakula, nishati na ufadhili, huku akikumbusha kwamba "suluhisho lolote la maana kwa ukosefu wa chakula duniani linahitaji kuunganisha tena uzalishaji wa mazao ya kilimo wa Ukraine na uzalishaji wa chakula na mbolea wa Russia na Belarus katika masoko ya Dunia - licha ya vita."

Miwsho, ni "muhimu zaidi kuliko hapo awali" kwa wafadhili kufadhili kikamilifu mahitaji ya kibinadamu kwa msaada rasmi wa maendeleo.

David Beasley, Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, amezungumzia sana juu ya "dhoruba kamili" ambazo husababisha njaa, ambazo ni pamoja na migogoro, mabadiliko ya tabianchi na janga la UVIKO-19.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) Qu Dongyu amezungumzia umuhimu wa watu, amani, ustawi na Sayari ya Dunia.

"Duniani kote, ustawi unarudishwa nyuma," amesema. "Kuna usalama mdogo wa chakula, afya na kipato" huku ukosefu wa usawa unakuwa mkubwa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha