Kuwait yarejesha Misri mabaki ya kale ya sanaa tano za Kifarao yaliyoingizwa kwa magendo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 17, 2022
Kuwait yarejesha Misri mabaki ya kale ya sanaa tano za Kifarao yaliyoingizwa kwa magendo
Sanaa ya kale ya Kifarao iliyoingizwa kwa magendo ikionyeshwa wakati wa makabidhiano yaliyofanyika Kuwait City, Kuwait, Juni 16, 2022. Afisa mmoja wa Serikali ya Kuwait amesema, Alhamisi wiki hii nchi hiyo imerejesha kwa Misri mabaki ya sanaa za kale tano za Kifarao zilizoingizwa kwa magendo. (Picha na Asad/Xinhua)

KUWAIT CITY – Kuwait Alhamisi wiki hii imerejesha kwa Misri mabaki ya kale ya sanaa tano za Kifarao zilizoingizwa kwa magendo.

Mkuu wa Idara ya Sanaa na Makumbusho katika Baraza la Taifa la Sanaa, Utamaduni na Fasihi la Kuwait (NCCAL), Sultan Al-Duwaish amemkabidhi Balozi wa Misri nchini Kuwait sanaa hizo za kale kwenye Makumbusho ya Taifa ya Kuwait.

“Mabaki hayo ya kale ya Sanaa kutoka Misri yalisafirishwa kimagendo kutoka Misri Mwaka 2019 na kukamatwa na Idara ya Forodha katika Uwanja wa Ndege wa Kuwait,” Al-Duwaish amesema.

Ameeleza kuwa, vyombo kadhaa vya Serikali ya Kuwait, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje, Idara ya Forodha ya uwanja wa ndege na NCCAL, wameshirikiana na Ubalozi wa Misri nchini Kuwait kuchunguza na kurejesha mabaki haya kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa.

“Haya ni makabidhiano ya pili ya mabaki ya kihistoria kutoka Kuwait hadi Misri,” amesema, akiongeza kwamba sanaa ya kale ya kwanza kurejeshwa ilikuwa ni mfuniko wa jeneza la mbao.

Balozi wa Misri nchini Kuwait Osama Shaltout amepongeza mchango wa vyombo vya Serikali ya Kuwait na juhudi zao zisizo na kuchoka katika kurudisha sanaa za kale kwenye asili yake.

“Vitu hivi vitarejeshwa Misri na vitafanyiwa uchunguzi zaidi ili kubaini umuhimu wake,” amesema balozi huyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kuwait, vitu vinne kati ya vitu hivyo vitano vilivyokamatwa nchini Kuwait vilikuwa sanamu za Mafarao wa Misri, ikiwemo Amenhotep III, Amun-Ra na mungu wa kale wa Misri Horus, pamoja na mchoro wa mawe.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha