Bunge la Israel lavunjwa, Lapid kuwa Waziri Mkuu wa muda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 01, 2022

Waziri Mkuu wa Israel anayemaliza muda wake Naftali Bennett (kulia) na Waziri Mkuu mpya Yair Lapid (wa pili kulia) wanaonekana wakiwa pamoja bungeni wakati wa kipindi cha majadiliano na kupiga kura kuhusu mswada wa kulivunja Bunge la Israel mjini Jerusalem, Tarehe 30 Juni, 2022. Wabunge wa Israel Alhamisi wiki hii wamepiga kura ya kulivunja bunge, kuhitimisha serikali ya mseto iliyodumu kwa mwaka mmoja ya Waziri Mkuu Naftali Bennett na kuirejesha nchi hiyo kwenye uchaguzi kwa mara ya tano ndani ya muda usiozidi miaka minne, hatua ambayo inaweza kumfanya Waziri Mkuu wa zamani Benjamin Netanyahu kurejea madarakani. (JINI kupitia Xinhua)

JERUSALEM - Wabunge wa Israel Alhamisi wiki hii wamepiga kura ya kulivunja bunge la nchi hiyo, kuhitimisha serikali ya mseto ya Waziri Mkuu Naftali Bennett iliyodumu kwa mwaka mmoja hivyo kuirejesha nchi hiyo kwenye uchaguzi kwa mara ya tano ndani ya muda usiozidi miaka minne, hatua ambayo inaweza kumfanya Waziri Mkuu wa zamani Benjamin Netanyahu kurejea madarakani.

“Bunge hilo lenye wabunge 120 lilipiga kura 92-0 kujivunjilia mbali na kuandaa uchaguzi ujao Novemba 1,” msemaji wa bunge amesema katika taarifa.

Bennett anatarajiwa kukabidhi madaraka kwa Yair Lapid, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel na kiongozi wa chama cha mrengo wa kati cha Yesh Atid, chini ya makubaliano ya kugawana madaraka waliyokubaliana kufuatia uchaguzi ambao haukuamua mshindi wa jumla Mwaka 2021.

Mabadiliko hayo ya uongozi yataanza rasmi kuanzia leo Ijumaa na Lapid atashikilia wadhifa huo hadi serikali ijayo itakapoundwa.

Lapid ambaye ni mwanahabari wa zamani na mhusika wa vyombo vya habari, atakuwa waziri mkuu wa 14 wa Israel, akichukua nafasi ya Bennett, kiongozi aliyetumikia nafasi yake kwa muda mfupi zaidi nchi humo.

Akiwa waziri mkuu wa muda, Lapid mwenye umri wa miaka 58, atakuwa na ratiba iliyojaa masuala ya kidiplomasia na usalama. Siku ya Jumapili, atakuwa mwenyeji wa mkutano wake wa kwanza wa baraza la mawaziri kama waziri mkuu. Siku mbili baadaye atasafiri kwenda Paris kukutana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Katikati ya Julai, ndiye atakutana na Rais wa Marekani Joe Biden, ambaye ziara yake ya Mashariki ya Kati iliyopangwa kabla inahusisha Israel na Saudi Arabia. Israel inatumai kuwa Ikulu ya Marekani, White House itasaidia kujenga ushirikiano wa kiusalama na Saudi Arabia dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ya Iran.

Waziri Mkuu wa Israel anayemaliza muda wake Naftali Bennett (wa pili kulia, mbele) na Waziri Mkuu mpya Yair Lapid (wa kwanza kulia, mbele) wanaonekana wakiwa pamoja bungeni wakati wa kipindi cha majadiliano na kupiga kura kuhusu mswada wa kulivunja Bunge la Israel mjini Jerusalem, Juni 30, 2022. (JINI kupitia Xinhua)

Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain katika eneo la Ghuba zilikubaliana kurejesha uhusiano wao na Israel Mwaka 2020 chini ya makubaliano ya Abraham yaliyosimamiwa na Marekani, lakini Saudi Arabia haijafanya hivyo.

Serikali hiyo ya Mseto iliyokuwa ikiongozwa na Bennett ilishinikiza kuidhinishwa kwa haraka mswada wa kuvunjwa kwake baada ya kutangaza wiki iliyopita kwamba serikali yake haiwezi tena kuwajibika.

Serikali hiyo ya mseto ilianza kazi Juni 2021, wakati Bennett na Lapid walipoungana kuunda Serikali baada ya miaka miwili ya mvutano wa kisiasa ambapo hakuna mgombea, akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, aliyeweza kupata kura za kutosha kumwezesha kuunda serikali peke yake.

Mlolongo wa wabunge kuhama kambi za kisiasa kumeufanya mseto huo wa vyama katika serikali kupoteza udhibiti wa bunge.

Hali hiyo sasa inampa nafasi kubwa Netanyahu na washirika wake kurejea kwenye uchaguzi wa baadaye Mwezi Novemba na pengine kurejea kwenye nafasi ya Waziri Mkuu. 

Waziri Mkuu wa zamani Benjamin Netanyahu (mbele) akizungumza bungeni wakati wa kipindi cha majadiliano na kupiga kura kuhusu mswada wa kulivunja Bunge la Israel mjini Jerusalem, Juni 30, 2022. (JINI kupitia Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha