

Lugha Nyingine
Rais wa Misri azindua majaribio ya reli ya kutumia umeme iliyojengwa na China
CAIRO - Mfumo wa kwanza wa reli ya kutumia umeme ya Misri (LRT) uliojengwa kwa pamoja na makampuni ya China na Misri ulianza majaribio yake siku ya Jumapili.
Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi alichukua usafiri wa kwanza wa LRT katika sherehe ya kuzinduliwa kwake, ambayo pia ilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Misri Mostafa Madbouly na Balozi wa China nchini Misri Liao Liqiang.
Mradi huo wa LRT ni matunda ya mkataba wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.24 uliotiwa saini Mwezi Agosti 2017 kati ya Mamlaka ya Taifa ya Mahandaki ya Misri (NAT) na muungano wa Kampuni ya Uhandisi wa Reli ya China na Kampuni ya Kimataifa ya AVIC (CREC-AVIC INTL Consortium).
Mradi huo wa reli unaunganisha Mji Mkuu Mpya wa Utawala wa Misri (NAC) unaojengwa Mashariki mwa Cairo na miji na wilaya mpya za mbali ikijumuisha miji ya El-Salam, Ramadan ya 10, El-Obour, Badr na El-Shorouk.
Waziri wa Uchukuzi wa Misri Kamel el-Wazir amesema awamu ya kwanza ya LRT ina treni 22 na itahudumia abiria 360,000 kila siku.
Mpangilio wa vituo 12 vya LRT unaanzia kituo kikuu cha Adly Mansour, ambacho ni kitovu cha usafirishaji Mashariki mwa Cairo, na kuishia NAC, ikijumuisha madaraja saba, mahandaki matatu, vituo vidogo viwili na depo moja.
Mradi huo wa LRT umegawanywa katika awamu kadhaa, ukichukua jumla ya umbali wa kilomita 103 na vituo 19.
El-Wazir amesema, awamu ya sasa ambayo imezinduliwa inashughulikia umbali wa takriban kilomita 70 na vituo 12. Awamu za baadaye zitajumuisha upanuzi wa Kusini ambao unachukua umbali wa karibu kilomita 18.5 na vituo vinne na upanuzi wa Kaskazini ambao unachukua takriban kilomita 16 na vituo vitatu.
Kwa mujibu wa waziri huyo, takriban makampuni 20 ya Misri na 15 ya China yalishiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
"Mradi huo umefadhiliwa na China, umetumia teknolojia na vifaa vya China, na umetekelezwa kwa pamoja na makampuni ya China na Misri," Liao amesema, akiongeza kuwa washiriki wote walijitahidi kuzingatia maendeleo ya ujenzi huku wakipambana dhidi ya janga la UVIKO-19.
Hassan Mahdy, profesa wa uchukuzi na barabara katika Chuo Kikuu cha Ain Shams cha mjini Cairo, amesema kuwa LRT ni muhimu sana kwani inaunganisha miji mipya ya Mashariki mwa Cairo, ikiwa ni pamoja na NAC, na wilaya zote za Cairo Kuu.
"Inanufaisha pande zote mbili, kwani ni huduma inayohitajika nchini Misri na ninaamini upande wa China una nia ya kuhamisha teknolojia zake husika na kupanua soko la bidhaa zake za usafirishaji. Kwa hivyo, ni mradi wa kunufaishana," profesa huyo ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma