Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia atembelea Misri ikiwa ni ziara ya kwanza barani Afrika tangu mgogoro kati ya Russia na Ukraine

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 25, 2022
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia atembelea Misri ikiwa ni ziara ya kwanza barani Afrika tangu mgogoro kati ya Russia na Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Shoukry (Kulia) akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov mjini Cairo, Misri, Julai 24, 2022. (Picha na Ali Bob/Xinhua)

CAIRO - Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi Jumapili amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov aliyezuru mjini Cairo, ambapo walijadili uhusiano wa pande mbili na masuala ya kikanda na kimataifa yanayoathiri pande mbili.

Ikulu ya Misri imesema katika taarifa kuwa, Lavrov amemkabidhi Sisi barua kutoka kwa Rais wa Russia Vladimir Putin, ikielezea kwamba Russia inaweka umuhimu mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Misri ndani ya mfumo wa "mkataba wa ubia na ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili,"

Sisi amepongeza ushirikiano unaokua kati ya Cairo na Moscow, ambao unadhihirishwa na miradi ya Russia nchini Misri, kama vile kinu cha nyuklia cha El-Dabaa ambacho kinajengwa hivi sasa, na uanzishwaji wa eneo maalumu la viwanda la Russia kwenye mhimili wa Mfereji wa Suez na miradi mingine ya pamoja katika nyanja mbalimbali.

Kuhusiana na mgogoro unaoendelea kati ya Russia na Ukraine, Misri imesisitiza wito wake wa suluhu ya kisiasa ya mgogoro huo.

Sisi amesisitiza "umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa mazungumzo na ufumbuzi wa kidiplomasia kwa mgogoro," akithibitisha uungaji mkono wa Misri kwa jitihada zote ambazo zitatatua suala hilo "kisiasa" ili kudumisha usalama na utulivu wa kimataifa.

Ni ziara ya kwanza ya Lavrov barani Afrika tangu kuanza kwa vita kati ya Russia na Ukraine vilivyoanza mwishoni mwa Februari. Lavrov amepanga pia kuzuru Ethiopia, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baada ya mazungumzo yake na Sisi, Lavrov alifanya mkutano na mwenzake wa Misri Sameh Shoukry kwenye makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri mjini Cairo.

Lavrov alisema amekuwa na "mazungumzo ya kiujenzi" na Rais wa Misri na baadaye na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Misri, akielezea shukrani za Russia kutokana na kukua kwa kasi kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya kukutana na Shoukry, Lavrov amesema kuwa, Russia na Misri zina msimamo wa pamoja kuhusu masuala mengi ya kikanda na kimataifa, yakiwemo mgogoro kati ya Palestina na Israel na migogoro ya Syria, Libya na Iraq.

Kuhusu uhaba wa chakula duniani unaotokana na mgogoro kati ya Russia na Ukraine, Lavrov amelaumu vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia vinavyozuia kusafirisha nafaka, akibainisha kuwa Russia na Ukraine hivi karibuni zimetia saini makubaliano ya kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa chakula kupitia kutenga kanda salama kwenye Bahari Nyeusi kwa ajili ya usafirishaji wa nafaka.

Lavrov amebainisha kuwa ziara yake barani Afrika pia inalenga kujadili maandalizi ya mkutano wa pili wa kilele kati ya Russia na Afrika ambao umepangwa kufanyika katikati ya Mwaka 2023. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha