Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa asema lengo la kukomesha UKIMWI ifikapo Mwaka 2030 liko "nje ya njia"

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 01, 2022

UMOJA WA MATAIFA - Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Korosi Jumatano alitoa wito wa kuchukua hatua kwani lengo la kukomesha UKIMWI ifikapo Mwaka 2030 liko "nje ya njia"

Katika ujumbe wake kwa Siku ya Ukimwi Duniani, ambayo inaadhimishwa leo Desemba 1 duniani kote, Korosi amesema lengo la kukomesha UKIMWI ifikapo Mwaka 2030 haliko sawa, kwani "kukosekana kwa usawa, kuwa na ubaguzi, na kutozingatiwa kwa haki za binadamu kunakwamisha maendeleo yetu."

"Lazima tushughulikie changamoto hizi ambazo zimeweka VVU/UKIMWI kuwa janga la afya duniani kwa zaidi ya miaka 40," amesema.

Kuna njia ya kisayansi ya kukomesha UKIMWI, lakini cha kusikitisha ni kwamba haipatikani kwa wote, amesema.

Iwapo jumuiya ya kimataifa itachukua hatua, maambukizi mapya ya VVU milioni 3.6 na vifo milioni 1.7 vinavyohusiana na UKIMWI vitazuiliwa katika muongo huu, amesema.

Tamko la Kisiasa la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Mwaka 2021 kuhusu UKIMWI linajumuisha ahadi na shabaha za kimataifa kwa Mwaka 2025 ambazo ni kabambe, lakini zinazoweza kufikiwa na serikali na jamii, amesema Korosi, huku akitoa wito kwa nchi wanachama na washikadau kuhuisha ahadi zao za kisiasa na kifedha ili kukomesha UKIMWI.

"Lazima tuhakikishe upatikanaji wa huduma zenye ushahidi wa kisayansi kwa wote, kama vile upimaji na matibabu, pamoja na ushirikiano wa kimataifa kuhusu teknolojia mpya," amesema.

Mshikamano wa kimataifa katika mfumo wa ufadhili endelevu pia unahitajika sana. Iwapo juhudi zitafanywa kusawazisha, Dunia itarejea kwenye njia ili kusiwe na mtu atakayeachwa nyuma, amesema. "Janga la UKIMWI liko tayari kwa ufumbuzi unaozingatia sayansi, mshikamano na uendelevu. Ninakaribisha kila mtu kujiunga na wito huo na kuchukua hatua."

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha