Viongozi mbalimbali duniani waomboleza kifo cha kiongozi wa zamani wa China Jiang Zemin

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 02, 2022

BEIJING - Viongozi wa nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa wametoa salamu zao za rambirambi kwa njia ya simu, barua na njia nyinginezo kwa Rais wa China Xi Jinping kutokana na kufariki dunia kwa kiongozi wa zamani wa China Jiang Zemin.

Akisisitiza kujitolea muhimu kwa Jiang kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya China ya sasa na kupanda kwa nchi hiyo katika hadhi ya kimataifa, Rais wa Russia Vladmir Putin amesema Jiang alikuwa rafiki mkubwa wa Russia, ambaye alitoa mchango mkubwa katika kuinua uhusiano kati ya Russia na China katika ushirikiano wa kimkakati wa uratibu.

Jiang alitoa mchango muhimu kwa ajili ya ujamaa wenye umaalumu wa China, amesema Thongloun Sisoulith, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi cha Laos (LPRP) na Rais wa Laos.

Jiang alikuwa mwanasiasa bora na kiongozi wa kikomunisti, na pia ni rafiki wa karibu wa Mapinduzi ya Cuba, amesema Miguel Diaz-Canel Bermudez, Katibu wa Kwanza wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Cuba na Rais wa Cuba, huku akiongeza kuwa Cuba inatoa rambirambi zake za dhati kwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), serikali na watu wa China.

Jiang ameiongoza China katika kipindi cha ukuaji wa haraka wa uchumi na maendeleo kupitia mageuzi endelevu ya kiuchumi, amesema Rais wa Singapore Halimah Yacob, huku akiongeza kuwa mawazo yao yako pamoja na watu wa China wakati huu wa majonzi.

Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev amesema Jiang alijitolea kuhimiza maendeleo na ustawi wa China, na kuongeza ushawishi wake kimataifa.

Kiongozi huyo wa zamani wa China alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha urafiki kati ya Kazakhstan na China, na atakumbukwa milele na watu wa nchi hizo mbili, ameongeza.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amesema yeye na wananchi wa Palestina daima watamkumbuka Jiang Zemin kama kiongozi bora ambaye alikuwa muungaji mkono wa watu wa Palestina na mapambano yao na haki zao za kisheria, mhamasishaji wa uhusiano kati ya Palestina na China na shahidi aliyeshuhudia kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa CPC, watu wa China na familia ya Jiang.

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida amesema Jiang alihimiza mageuzi na ufunguaji mlango wa China, alitoa mchango kwa maendeleo ya China na alichukua nafasi muhimu katika kuhimiza maendeleo ya uhusiano kati ya Japan na China.

Viongozi wengine waliotoa salamu za rambirambi zenye ujumbe mbalimbali wa kumkumbuka na kuthamini mchango mkubwa wa Jiang Zemin ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Waziri Mkuu wa Cambodia Samdech Techo Hun Sen, Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel, Rais wa Nicaragua, Daniel Ortega, Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko, Rais wa Moldova, Ibrahim Mohamed Solih na wengine wengi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha