Magonjwa ya kupumua yaenea kote Marekani, na kuzidisha mzigo kwenye hospitali

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 06, 2022
Magonjwa ya kupumua yaenea kote Marekani, na kuzidisha mzigo kwenye hospitali
Mhudumu wa afya akipima halijoto ya wageni katika hospitali ya New York, Marekani, Desemba 13, 2021. (Xinhua/Wang Ying)

LOS ANGELES - Marekani inakabiliwa na ongezeko la magonjwa ya mfumo wa kupumua ikiwa ni pamoja na UVIKO-19, mafua na virusi vya kupumua (RSV), na hivyo kuzidisha mzigo katika hospitali.

Maambukizi ya mafua ya msimu yako katika kiwango cha juu na yanaendelea kuongezeka kote nchini humo, kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC).

Jumla ya serikali za majimbo na mitaa 47 za Marekani zimeshuhudia maambukizi ya mafua "ya juu" au "juu sana" katika wiki iliyoishia Novemba 26, kutoka maeneo 36 ya kiserikali wiki moja kabla, takwimu za CDC zimeonyesha. Takriban watu 20,000 waliolazwa hospitalini kutokana na mafua waliripotiwa kote nchini katika wiki hiyo.

Kumekuwa na angalau wagonjwa milioni 8.7, waliolazwa hospitalini 78,000, na vifo 4,500 kutokana na mafua hadi sasa msimu huu nchini Marekani, kwa mujibu wa CDC.

Miongoni mwao, jumla ya vifo 14 vya mafua ya watoto viliripotiwa.

Maafisa wa afya wameonya kuwa Marekani inapaswa kutarajia msimu mbaya zaidi wa mafua, kwani majira ya baridi haya yatakuwa ya kwanza ambapo watu wengi watarejea kuishi maisha ya kawaida baada ya tahadhari za UVIKO.

Wataalamu wa afya wameonya juu ya "janga la mara tatu" linaloikabili nchi hiyo huku UVIKO-19 ukiendelea, na visa vya mafua na RSV kuongezeka.

Marekani ilikuwa na wastani wa wagonjwa wa kulazwa hospitalini kwa kila siku 4,200 wa UVIKO-19 katika wiki iliyoishia Novemba 29, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.6 kutoka wiki moja iliyopita.

Hospitali za UVIKO wiki iliyopita zilifikia kiwango chao cha juu zaidi katika miezi mitatu, na zaidi ya wagonjwa 35,000 wakitibiwa, kwa mujibu wa ufuatiliaji wa takwimu wa Washington Post.

Wataalam wanasema kuwa mikusanyiko ya likizo ni wakati mzuri kwa virusi vya Korona kuenea wakati mamilioni ya Wamarekani wanasafiri na kukusanyika.

"Inaweza kuwa katika wiki moja au mbili tunaona wagonjwa wengi zaidi wa UVIKO kuliko tunavyoona RSV au mafua, lakini wasiwasi halisi ni kwamba tutaona wimbi kubwa la wote wakiupa shinikizo kubwa sana uwezo wa hospitali kuwahudumia hawa wagonjwa wanaoumwa sana," Nancy Foster wa Jumuiya ya Hospitali ya Marekani amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha