Kenya yapokea mabehewa mapya kutoka China kwa usafirishaji wa mizigo wa reli

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 05, 2024

MOMBASA - Kenya imepokea mabehewa 430 kutoka China siku ya Jumatatu ili kuimarisha shughuli zake za usafirishaji wa mizigo wa reli nchini kote. Kundi hilo la mabehewa linajumuisha mabehewa 230 yaliyoundwa kwa ajili ya njia ya Reli ya Standard Gauge (SGR) iliyojengwa na China na mabehewa 200 kwa njia ya Reli ya Meter Gauge.

Mohamed Daghar, Katibu Mkuu katika Wizara ya Barabara na Uchukuzi ya Kenya, amesema mabehewa hayo yataimarisha usambazaji wa mizigo kutoka bandari ya Mombasa na kusaidia kupunguza foleni barabarani.

"Ikizingatiwa kuwa uchumi wa Kenya ni mojawapo ya uchumi unaokua kwa kasi katika ukanda huu, tunatakiwa kufanya uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji ili kuhakikisha kuwa usafirishaji wa mizigo unatekelezwa ipasavyo kwa ufanisi," Daghar amesema wakati akipokea mabehewa hayo katika bandari ya Mombasa.

Philip Mainga, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli la Kenya, amesema kuwa kitengo cha usafirishaji cha shirika hilo kimesaini mikataba ya muda mrefu ya usafirishaji wa mizigo na wateja kadhaa na kimeweka mipango ya kuhakikisha kwamba kinatoa huduma ya kuaminika, salama na yenye ufanisi.

“Kwa jumla, tunanunua mabehewa 500 ambayo yanajumuisha mabehewa 300 yaliyoundwa kwa ajili ya uendeshaji wa njia ya Reli ya Standard Gauge na mabehewa 200 yaliyoundwa kwa ajili ya uendeshaji wa njia ya Reli ya Meter Gauge,” Mainga amesema. "

Kuwasili kwa mabehewa hayo mapya kunakuja takribani mwezi mmoja baada ya Kenya kupokea mabehewa mapya 50 kutoka China ili kurahisisha shughuli za huduma ya usafirishaji wa shehena ya SGR mwezi Februari.

Takwimu kutoka Wizara ya Uchukuzi ya Kenya zinaonyesha ongezeko la asilimia 21 la mizigo iliyosafirishwa kupitia reli ya meter gauge kutoka tani 787,000 mwaka 2022 hadi tani 1,000,955 mwaka 2023. Zaidi ya hayo, mizigo iliyosafirishwa kupitia SGR iliongezeka kwa asilimia 7 hadi tani milioni 6.53 Mwaka 2023 kutoka tani milioni 6.53 Mwaka 2022, huku idadi ya abiria pia ikiongezeka kwa asilimia 12 hadi kufikia milioni 2.73 kutoka milioni 2.39 Mwaka 2022.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Deng Jie)

Picha