Wataalamu wa Afrika wakutana nchini Kenya kuyapa kipaumbele malengo ya mabadiliko ya tabianchi duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 10, 2024

NAIROBI - Wataalamu wa Afrika wamekutana mjini Nairobi, Kenya, siku ya Jumanne ili kusawazisha vipaumbele vyao na malengo ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mwezi Juni mwaka huu nchini Ujerumani.

Mkutano huo wa siku nne, unaowakutanisha pamoja watunga sera, wafanya majadiliano, watendaji, mashirika ya wakulima, na mashirika ya kiraia kutoka nchi 30 za Afrika, utaweka msimamo wa pamoja wa Afrika kabla ya mkutano wa 60 wa Chombo Tanzu cha Ushauri wa Sayansi na Teknolojia na Chombo Tanzu cha Utekelezaji (SB 60) utakaofanyika tarehe 3 hadi tarehe 13 Juni mwaka huu huko Bonn.

Katika hotuba yake, George Wamukoya, kiongozi wa timu ya Kundi la uungaji mkono wa Wataalamu wa Majadiliano la Afrika (AGNES), amesema kuwa ni muhimu kwamba wataalam waweze kuungana chini ya msimamo wa pamoja wa Afrika ili kuandaa mazingira kwa ajili ya kuchukua hatua zenye maana katika mikutano ijayo ya mabadiliko ya tabianchi.

"Juhudi za pamoja, zikiongozwa na kutafakari matokeo ya COP28, zitaunda mbinu za kimkakati katika kilimo, kukabiliana na hali za mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia, afya, usalama wa maji, bioanuwai, na ufumbuzi unaojikita katika mazingira asilia," Wamukoya amesema kwenye ufunguzi wa mkutano huo.

Ameongeza kuwa, kwa njia ya mazungumzo, ushirikiano, na azma, kuna udharura wa kuandaa njia kuelekea maendeleo yenye unyumbufu, uendelevu, na uwiano kwa bara zima.

Mkutano huo unatarajiwa kuwapa wafanya majadiliano wa Afrika mkakati na mbinu ya kushiriki katika mazungumzo ya kilimo, kukabiliana na hali, hasara na uharibifu wa mabadiliko ya tabianchi, na ufadhili wa kuwezesha kukabiliana na hali.

Mithika Mwenda, mkurugenzi mtendaji wa Muungano wa Haki za Mabadiliko ya Tabianchi wa Africa (PACJA), ameahidi kutumia ushawishi wake wa kualika wadau na kuandaa mikutano kuwezesha mashauriano mapana kuhusu masuala ya kukabiliana na hali ya mabadiliko ya tabianchi katika mikutano ya 60 ya SB 60 mjini Bonn.

Wakati huo huo, Anne Wang'ombe, katibu mkuu katika Wizara ya Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi wa Kenya, amewataka wataalam hao wa mabadiliko ya tabianchi barani Afrika wajumuishe mitazamo ya kijinsia ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika bara hilo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha