

Lugha Nyingine
Waziri wa Mambo ya Nje wa China akutana na mabalozi wa Afrika
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akikutana na mabalozi wa Afrika nchini China na kuadhimisha kwa pamoja Siku ya Afrika mjini Beijing, mji mkuu wa China, Mei 26, 2025. (Xinhua/Yue Yuewei)
BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amekutana na mabalozi na wajumbe wa Afrika nchini China jana Jumatatu na kuadhimisha Siku ya Afrika pamoja mjini Beijing ambapo mabalozi au makaimu mabalozi wa zaidi ya nchi 50 za Afrika nchini China na wawakilishi wa Umoja wa Afrika nchini China walihudhuria mkutano huo.
Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amesema tangu kuingia kwenye zama mpya, Rais Xi Jinping ametembelea Afrika mara tano na kuweka mbele kanuni ya sera ya China kuhusu Afrika - udhati, matokeo halisi, upendo na nia njema, na kanuni ya kutafuta maslahi makubwa zaidi na ya pamoja, vilevile moyo wa urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika, ikiinua uhusiano wa pande mbili kati ya China na nchi zote za Afrika kwenye ngazi ya uhusiano wa kimkakati.
"Nafasi ya jumla ya uhusiano kati ya China na Afrika pia imepandishwa hadhi na kuwa jumuiya ya hali zote ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya, na uhusiano wa China na Afrika umeingia katika kipindi bora zaidi katika historia," Wang ameongeza.
Wang amesema, kwenye Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika Beijing Septemba mwaka jana, Rais Xi alitoa mapendekezo sita na hatua 10 za ushirikiano kwa ajili ya kuhimiza kwa pamoja ujenzi wa mambo ya kisasa.
"China inapenda kutumia mkutano ujao wa mawaziri wa waratibu kwa ajili ya utekelezaji wa matokeo ya baraza hilo kama fursa ya kutekeleza maafikiano yaliyofikiwa na viongozi wa pande zote mbili, kuweka kigezo cha ushirikiano wa kiwango cha juu chini ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, kujenga muundo wa kutekeleza Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, na kuharakisha ujenzi wa pamoja wa mambo ya kisasa wa China na Afrika," Wang amesema.
Amebainisha kuwa, kadiri hali ya kimataifa inavyozidi kuwa na misukosuko, ndivyo China na Afrika zinavyohitaji kuimarisha mshikamano na ushirikiano zaidi, kwa pamoja kupinga siasa za umwamba, kutetea ushirikiano wa pande nyingi, kulinda mfumo wa kimataifa huku Umoja wa Mataifa ukiwa ndiyo msingi wake, na kwa pamoja kuhimiza biashara na uwekezaji kuwa huria na rahisi .
"China, kama ilivyo wakati wote, bila kuyumbayumba itaunga mkono msimamo wa haki wa nchi za Afrika na kithabiti inaiunga mkono Afrika katika kutoa mchango mkubwa zaidi katika jukwaa la kimataifa," Wang amebainisha.
Wajumbe hao wa Afrika wamesema kuwa nchi za Afrika zimetiwa moyo sana na mfululizo wa mapendekezo ya kimataifa na hatua 10 za ushirikiano zilizopendekezwa na Rais Xi, na zimejaa imani katika ushirikiano kati ya Afrika na China.
"Nchi za Afrika zinafuata kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja, kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na China kulinda mamlaka yake na kufikia muungano wa kitaifa, na kupinga uingiliaji wa mambo ya ndani ya China," wamesema wajumbe hao, wakiongeza kuwa nchi za Afrika kwa pamoja zitalinda madhumuni na kanuni za Katiba ya Umoja wa Mataifa, na kulinda maslahi ya pamoja ya kundi la Nchi za Kusini pamoja na China.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akikutana na mabalozi na wajumbe wa Afrika nchini China na kuadhimisha pamoja Siku ya Afrika mjini Beijing, mji mkuu wa China, Mei 26, 2025. (Xinhua/Yue Yuewei)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma