Makumi ya watu wajeruhiwa baada ya gari kuparamia umati wa watu kwenye matembezi ya Liverpool

(CRI Online) Mei 27, 2025

Idara ya Huduma ya Dharura ya Kaskazini Magharibi ya Uingereza imesema kuwa makumi ya watu, wakiwemo watoto wanne wamejeruhiwa baada ya gari moja kuparamia umati wa watu katikati ya mji wa Liverpool wakati maelfu ya watu wakisherehekea ubingwa wa klabu ya soka ya Liverpool wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mkuu Msaidizi wa polisi Bi. Jenny Sims amewaambia wanahabari kuwa jumla ya watu 27 wamepelekwa hospitali, huku wawili kati yao wakiwa wamejeruhiwa vibaya, ikiwa ni pamoja na mtoto mmoja.

Ameeleza kuwa, tukio hilo halichukuliwi kama kitendo cha ugaidi.

Muingereza mwenye umri wa miaka 53 amekamatwa na anaaminika kuwa dereva wa gari hilo.

Gari hilo lilisimamishwa haraka kwenye eneo la tukio, na mshukiwa wa kiume alipelekwa korokoroni haraka.

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema katika taarifa kufuatia tukio hilo kuwa mkasa huo wa Liverpool ni wa kutisha, na moyo wake uko pamoja na wale wote waliojeruhiwa au walioathirika.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha