Kenya yafungua ubalozi wa kwanza nchini Morocco ikiashiria mabadiliko ya sera juu ya mzozo wa Sahara Magharibi

(CRI Online) Mei 27, 2025

Kenya imefungua ubalozi wake wa kwanza nchini Morocco jana Jumatatu wakati nchi hizo mbili zikiadhimisha miongo sita ya uhusiano wa kidiplomasia, hatua ambayo inasisitiza uhusiano wa kina na mabadiliko makubwa katika mzozo wa Sahara Magharibi.

Hafla ya ufunguzi wa ubalozi huo iliyofanyika Rabat ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Nasser Bourita na Mkuu wa Mawaziri wa Baraza la Mawaziri la Kenya ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni na Diaspora Musalia Mudavadi.

Katika ziara rasmi ya siku mbili ya Mudavadi iliyoanza Jumatatu, nchi hizo mbili zimesaini hati tano za maelewano zinazolenga kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya makazi na miji, masuala ya vijana, mafunzo ya kidiplomasia, kukuza biashara na kujenga uwezo wa utumishi wa umma.

Kenya pia imeidhinisha rasmi Mpango wa Kujitawala wa Morocco kama "njia pekee endelevu" ya kusuluhisha mzozo wa Sahara Magharibi, ikiwa ni mabadiliko makubwa ya sera ya Nairobi juu ya mzozo huo.

Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ulikuwa umedorora kwa miaka mingi kutokana na Kenya kuunga mkono harakati ya Polisario Front na kuitambua kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Waarabu ya Sahrawi (SADR), ambayo inataka uhuru wa Sahara Magharibi kutoka kwa Morocco.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha