

Lugha Nyingine
IGAD yaonya kupanda kwa joto huko Pembe ya Afrika
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa (ICPAC) kilichoko chini ya Mamlaka ya Kiserikali kwa Maendeleo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD), joto linatarajiwa kupanda zaidi ya kawaida katika nchi zisizopungua saba za Pembe ya Afrika kati ya Juni na Agosti.
Kwenye tahadhari iliyotolewa jana Jumatatu mjini Nairobi, ICPAC imesema nchi hizo ni Ethiopia, Somalia, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na Tanzania na kwamba baadhi ya nchi zitashuhudia nyuzi joto zaidi ya 32 sentigredi katika kipindi hicho, zikiwemo Ethiopia na Somalia.
Tahadhari hiyo pia imeainisha kuwa halijoto ya msimu inatarajiwa kupanda zaidi ya kawaida maeneo ya kaskazini, magharibi na mashariki ya kanda hiyo.
Kwa mujibu wa ICPAC, joto litaendelea kupanda licha ya kanda hiyo kutarajiwa kuwa na mvua nyingi zaidi ya kawaida katika kipindi hicho.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma