

Lugha Nyingine
Watalii 6 wafariki na wengine 27 wajeruhiwa katika ajali ya barabarani nchini Kenya
Mkuu wa Kaunti ya Nyandarua ya Kenya Bw. Abdrisack Jaldesa amesema watalii sita wamefariki na wengine 27 wamejeruhiwa katika ajali iliyotokea jana Jumatatu alasiri kwenye barabara yenye magari mengi katikati mwa Kenya.
Bw. Jaldesa amesema basi lililokuwa likiwasafirisha watalii hao kutoka Kaunti ya Nakuru hadi Maporomoko ya Maji ya Thomson mjini Nyahururu katika Kaunti ya Laikipia lilibingirika na kuangukia kwenye mtaro katika eneo la Gichaka, umbali wa kilomita 41 kusini mwa Nyahururu.
Bw. Jaldesa amesema majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyahururu, akiongeza kuwa bado haijafahamika watalii hao wanatoka wapi.
Mashuhuda wamesema basi hilo lilikuwa likisafiri wakati mvua ikinyesha na dereva alipoteza udhibiti kabla ya basi hilo kugonga mti na kubingirika mara kadhaa, ikisababisha vifo vya watu sita waliokuwa ndani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma