China na Afrika zasukuma utekelezaji wa matokeo ya Mkutano Kilele wa FOCAC wa Beijing

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 12, 2025
China na Afrika zasukuma utekelezaji wa matokeo ya Mkutano Kilele wa FOCAC wa Beijing
Mkutano wa Mawaziri wa Waratibu wa Utekelezaji wa Matokeo ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) ukifanyika Changsha, Mkoa wa Hunan, katikati mwa China, Juni 11, 2025. (Xinhua/Chen Sihan)

CHANGSHA - Wawakilishi wa China, nchi 53 za Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Afrika wamekutana Changsha, China jana Jumatano ili kuhimiza utekelezaji kamili wa matokeo yaliyofikiwa katika Mkutano wa Kilele wa Beijing wa Barazaf la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) ambapo kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Waratibu wa Utekelezaji wa Matokeo ya FOCAC, Waziri wa Mambo ya Nje wa China na mwenzake wa Jamhuri ya Kongo, Jean-Claude Gakosso walisoma barua za pongezi kutoka kwa wakuu wa nchi hizo mbili.

Jamhuri ya Kongo ni mwenyekiti mwenza wa Afrika wa FOCAC.

Rais Xi Jinping wa China ameeleza katika barua hiyo umuhimu wa mshikamano na ushirikiano kati ya China na Afrika na kutangaza hatua muhimu za kufungua mlango na kushirikiana zaidi na Afrika, ambazo Wang amesema zinatoa mwongozo muhimu kwa pande zote mbili wakati ambapo zikitafuta kwa pamoja kuhimiza maendeleo ya mambo ya kisasa na kujenga jumuiya kati ya China na Afrika ya hali zote yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya.

"FOCAC imekua kwa kasi katika miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, ikiufanya uhusiano kati ya China na Afrika upate maendeleo ya haraka zaidi na kuingia kipindi bora katika historia. Pande zote mbili zimepiga hatua madhubuti katika utekelezaji hatua 10 za ushirikiano kwa maendeleo ya mambo ya kisasa zilizotangazwa kwenye mkutano wa kilele wa FOCAC wa Beijing uliofanyika Septemba iliyopita," amesema Wang.

Amesema, China na Afrika, ikiwa nchi kubwa zaidi inayoendelea na bara lenye nchi nyingi zaidi zinazoendelea, mtawalia, zinaibuka kuwa nguvu kuu ya Nchi za Kusini.

"Zikikabiliwa na hali ya kimataifa yenye mabadiliko na msukosuko, China na Afrika zinapaswa kushikilia mshikamano na kujitegemea zaidi kuliko wakati mwingine wowote," amesema, akitoa wito kwa pande zote mbili kuitikia hali ya kutokuwa na uhakika duniani kwa uhusiano thabiti na wenye unyumbufu kati ya China na Afrika.

“Pande zote mbili zinapaswa kulinda mshikamano wa Nchi za Kusini, kutetea biashara huria ya kimataifa, kuunga mkono ushirikiano wa maendeleo wa kimataifa, kutetea utaratibu wa kimataifa ulio wa haki na kuhimiza uanuwai wa kiustaarabu,” amesema.

Wang amesema karne ya 21 kwa kiasi kikubwa ni karne ya Asia kama ilivyo ya Afrika, akiongeza kuwa, maadamu watu zaidi ya bilioni 2.8 wa China na Afrika watafanya kazi pamoja, bila shaka watapata maendeleo makubwa katika njia ya kujipatia maendeleo ya mambo ya kisasa.

Kwa niaba ya nchi za Afrika, Gakosso amesema nchi za Afrika zinaishukuru China kwa kuunga mkono maendeleo yao, kukaribisha hatua 10 za ushirikiano wa maendeleo ya mambo ya kisasa, na kuunga mkono Dira ya Ushirikiano kati ya China na Afrika ya 2035.

Ameongeza kuwa nchi za Afrika zinapenda kutekeleza matokeo ya Mkutano wa Kilele wa Beijing ili kusaidia watu wa Afrika kufikia matarajio yao ya maisha bora.

"Upande wa Afrika unapinga hatua ya kutumia vibaya ushuru na vikwazo vya upande mmoja na utasimama na China kwa pamoja kukabiliana na changamoto," Gakosso amesema.

Mkutano huo umetoa Azimio la Changsha la China na Afrika juu ya Kushikilia Mshikamano na Ushirikiano wa Nchi za Kusini.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha