Maonyesho ya China na Asia Kusini yafunguliwa kwa kufuatilia biashara, viwanda vinavyoibukia (6)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 20, 2025
Maonyesho ya China na Asia Kusini yafunguliwa kwa kufuatilia biashara, viwanda vinavyoibukia
Wageni wakihudhuri hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya 9 ya China na Asia Kusini mjini Kunming, Mkoani Yunnan, kusini-magharibi mwa China, tarehe 19 Juni 2025. (Xinhua/Chen Xinbo)

KUNMING - Maonyesho ya 9 ya China na Asia Kusini yamefunguliwa jana Alhamisi mjini Kunming, mji mkuu wa Mkoa wa Yunnan, kusini-magharibi mwa China, yakivutia wawakilishi kutoka nchi, maeneo na mashirika ya kimataifa 73, vilevile kampuni za kiviwanda zaidi ya 2,500.

Kwa mujibu wa waandaaji na waratibu, maonyesho hayo ya siku sita yameleta pamoja nchi zote za Asia Kusini na Kusini-Mashariki, yakiwa na kumbi 16 za maonyesho, karibu asilimia 70 kati ya hizo zimetengwa kwa sekta za kitaalamu kama vile viwanda, nishati ya kijani, uzalishaji wa kahawa, na dawa za jadi za China.

Aidha, maeneo mawili yenye mambo na bidhaa za Asia Kusini yenye vibanda takriban 800 yamewekwa, huku India na Pakistan kila moja ikiwa na vibanda 140.

Waandaaji wameeleza kuwa, shughuli takriban 40 za kiuchumi na kibiashara yamepangwa wakati wa maonyesho hayo, yakiwemo ya mabaraza na mikutano ya kupatanisha wanunuzi inayolenga kuimarisha kwa kina ushirikiano wa kikanda.

Maonyesho hayo yalifanyika kwa mara ya kwanza Kunming mwaka 2013, mwaka huo huo ambao China ilitoa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja. Tangu wakati huo yamewezesha dola za Kimarekani zaidi ya bilioni 110 katika miamala ya biashara ya nje na kuhudumia kampuni za kiviwanda zaidi ya 20,000.

Yakiwa yanaandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Biashara ya China na serikali ya mkoa wa Yunnan, Maonyesho hayo yanatumika kama jukwaa muhimu la kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Asia Kusini.

Takwimu kutoka wizara hiyo zinaonesha kuwa, mwaka 2024, biashara kati ya China na nchi za Asia Kusini ilifikia karibu dola za Kimarekani bilioni 200, ikiongezeka mara mbili katika muongo mmoja uliopita kwa wastani wa ukuaji wa mwaka wa asilimia 6.3.

Naibu Waziri wa Biashara wa China Yan Dong amesema China inaendelea kudhamiria kwa ufunguaji mlango wa ngazi ya juu na kuhimiza maendeleo ya mambo ya kisasa ya China kupitia maendeleo bora ya hali ya juu, mchakato ambao utaleta fursa muhimu za ushirikiano na nchi mbalimbali duniani zikiwemo zile za Asia Kusini.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha