Maonyesho ya 31 ya uwekezaji na biashara ya Lanzhou, China yavutia ushiriki wa kimataifa (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 07, 2025
Maonyesho ya 31 ya uwekezaji na biashara ya Lanzhou, China yavutia ushiriki wa kimataifa
Waonyeshaji wakiandaa chai kwa watembeleaji kwenye Maonyesho ya 31 ya Uwekezaji na Biashara ya Lanzhou ya China huko Lanzhou, Mkoa wa Gansu, kaskazini-magharibi mwa China, Julai 6, 2025 (Xinhua/Zhang Zhimin)

LANZHOU - Maonyesho ya 31 ya Uwekezaji na Biashara ya Lanzhou ya China yamefunguliwa rasmi jana Jumapili huko Lanzhou, mji mkuu wa Mkoa wa Gansu, kaskazini-magharibi mwa China, yakivutia viwanda na kampuni zaidi ya 2,000 vya ndani na nje ya China ambapo katika maonyesho hayo ya mwaka huu, Indonesia imeamuliwa kuwa nchi mgeni mheshimiwa.

Waandaaji wa maonesho hayo wamesema, idadi ya washiriki kwenye maonyesho hayo imezidi ile ya maonyesho yaliyopita, na washiriki wa nchi zaidi ya 20, zikiwemo Ujerumani, Hispania, Russia, Malaysia na Iran, wameshiriki kwenye maonesho hayo pamoja na washiriki kutoka miji, mikoa na mikoa inayojiendesha 18 ya China, vilevile Mkoa wa Utawala Maalum wa Hong Kong wa China.

Wamesema kuwa, maonyesho hayo yana sehemu nne za maonyesho yanayohusisha ushirikiano wa kimataifa wa Njia ya Hariri, mawasiliano ya kikanda, bidhaa za wanunuzi, na viwanda maalum vya Gansu -- zikionyesha bidhaa za utengenezaji zana, kemikali za petroli, dawa za kiviumbe, nyenzo mpya, nishati mpya, usafiri wa ndege na usafiri kwenye anga ya juu, kilimo, na taarifa za data, huku majukwaa na shughuli za biashara zaidi ya 30 yamepangwa katika wakati wa maonyesho hayo.

Balozi wa Indonesia nchini China Djauhari Oratmangun amesema kuwa kampuni 16 za Indonesia zimewasilisha kahawa, vyakula, kazi za mikono na batiki za kijadi kwenye maonesho hayo, na ameeleza matumaini yake kuwa nchi mbili Indonesia na China zitaongeza kwa kina ushirikiano katika nishati mbadala, kilimo cha kisasa na utalii wa kitamaduni.

Yakiwa ni maonesho makubwa ya uchumi ya kimataifa ya mkoa huo wa Gansu tangu mwaka 1993, maonyesho hayo mwaka huu yamepata makubaliano ya miradi 1,181 ya uwekezaji yenye thamani ya jumla ya yuan zaidi ya bilioni 650 (dola za kimarekani takriban bilioni 90.9) katika sekta za zana za nishati mpya, utengenezaji wa mazao ya kilimo, raslimali mpya na teknolojia ya kidigitali. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha