

Lugha Nyingine
Rais Xi atoa wito wa ujenzi wa mtandao wa mazungumzo na ushirikiano kati ya nchi za ustaarabu mbalimbali duniani
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping katika barua ya pongezi kwa Mkutano wa Mawaziri wa Mazungumzo ya Ustaarabu ya Kimataifa uliofunguliwa jana Alhamisi mjini Beijing amesema kuwa China inapenda kushirikiana na nchi nyingine katika kujenga mtandao wa mazungumzo na ushirikiano kati ya nchi za ustaarabu mbalimbali.
Xi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ameahidi kwamba China itajiunga pamoja na nchi nyingine kushikilia mawazo ya ustaarabu kuhusu usawa, kufundishana, mazungumzo na ujumuishaji, na kutekeleza Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia, ili kutoa msukumo mpya kwa maendeleo ya ustaarabu wa binadamu na maendeleo ya amani ya dunia.
"Hali asili ya Dunia ni yenye ustaarabu mbalimbali. Historia imetuonyesha kwamba ustawi wa ustaarabu na maendeleo ya binadamu haviwezekani kutengana na mawasiliano na kufundishana kati ya nchi za ustaarabu mbalimbali. " Rais Xi amesema katika barua hiyo.
Amesema, katika dunia ambayo mageuzi na misukosuko vimechanganyikana, na binadamu wanasimama katika njia panda mpya, kuna hitaji kubwa la ustaarabu kuvuka mifarakano kupitia mawasiliano, na kuvuka migongano kupitia kufundishana.
Pia ameelezea matumaini yake kwamba washiriki wa mkutano watajihusisha katika mazungumzo ya kina ili kujenga miafaka na kuchangia hekima na nguvu zao kwa lengo la kuhimiza maelewano na urafiki miongoni mwa watu, na kufikia kuishi pamoja kwa mapatano kati ya nchi za ustaarabu mbalimbali.
Ukiwa na kaulimbiu ya "Kulinda Ustaarabu Mbalimbali wa Binadamu kwa Amani na Maendeleo ya Dunia," mkutano huo wa siku mbili unaandaliwa kwa pamoja na Idara ya Uenezi ya Kamati Kuu ya CPC na Idara ya Kimataifa ya Kamati Kuu ya CPC.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma