

Lugha Nyingine
China na Marekani zadumisha mawasiliano ya karibu ya kiuchumi na kibiashara katika ngazi mbalimbali
BEIJING - China na Marekani zimedumisha mawasiliano ya karibu ya kiuchumi na kibiashara katika ngazi mbalimbali, He Yongqian Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China amesema jana Alhamisi kwenye mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akijibu swali kuhusu iwapo Waziri wa Biashara wa Marekani na maafisa wengine waandamizi wa biashara wa nchi hiyo watakutana na wajumbe wa China mapema mwezi Agosti.
"Tangu Mei mwaka huu, kwa kuongozwa na maafikiano yaliyofikiwa kati ya wakuu wa nchi za China na Marekani, timu za uchumi na biashara za nchi zote mbili zimefanya mazungumzo ya ngazi ya juu ya biashara mjini Geneva na London, zikianzisha makubaliano mjini Geneva na mfumokazi mjini London," msemaji huyo amesema, akiongeza kuwa timu hizo zimekuwa zikifanya kazi kutekeleza matokeo hayo, ambayo yametuliza uhusiano wa pande mbili wa kibiashara.
Amesema kuwa, ni matumaini kuwa Marekani itashirikiana na China katika mwelekeo mmoja, kutilia maanani kanuni za kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na ushirikiano wa kunufaishana, na kutumia vema utaratibu wa mashauriano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani wakati huohuo kuendelea kuimarisha mazungumzo na mawasiliano.
Msemaji huyo pia ametoa wito kwa upande wa Marekani kuchukua hatua madhubuti za kushikilia na kutekeleza maafikiano muhimu yaliyofikiwa kati ya wakuu wa nchi hizo mbili wakati wa mazungumzo yao ya hivi karibuni kwa njia ya simu, kwa lengo la kuhimiza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati China na Marekani ulio tulivu, mzuri na endelevu, na kuingiza uhakika na utulivu zaidi katika maendeleo ya uchumi wa dunia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma