Kampuni ya China kupandisha kiwango cha barabara muhimu inayounganisha eneo la kati na kaskazini mwa Uganda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 14, 2025

Rais Yoweri Museveni wa Uganda akizungumza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa kupandisha kiwango cha barabara ya Kayunga-Bbaale-Galiraya mjini Kayunga, Uganda, Julai 11, 2025. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xi

Rais Yoweri Museveni wa Uganda akizungumza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa kupandisha kiwango cha barabara ya Kayunga-Bbaale-Galiraya mjini Kayunga, Uganda, Julai 11, 2025. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

KAMPALA - Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameweka jiwe la msingi la mradi wa kupandisha kiwango cha Barabara ya Kayunga-Bbaale-Galiraya yenye urefu wa kilomita 87.6, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa eneo la kuunganisha kivuko na daraja, katika Wilaya ya Kayunga katikati mwa Uganda ambapo Rais Museveni, akiambatana na Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong, ameanzisha ujenzi huo utakaodumu kwa miaka miwili siku ya Ijumaa katika mji wa Kayunga.

Mradi huo, unaofanywa na Shirika la Barabara na Madaraja la China (CRBC), utapandisha kiwango cha barabara hiyo kutoka kiwango cha changarawe hadi kiwango cha lami, ukiboresha mawasiliano kati ya eneo la kati la Uganda na mikoa ya kaskazini na mashariki kupitia Ziwa Kyoga.

"Tumekuwa tukipanga kuijenga kwa muda mrefu. Ni barabara ya kimkakati, inayopunguza umbali kati ya kaskazini mwa Uganda na Kampala," Museveni amesema, akiongeza kuwa barabara zilizoboreshwa zitasaidia wakulima kusafirisha mazao yao hadi sokoni kwa urahisi zaidi.

Balozi wa China amesema China inapongeza na kuunga mkono Uganda kuzingatia maendeleo ya miundombinu, akisisitiza kwamba ujenzi wa barabara ni muhimu kwa uzalishaji mali wa nchi.

"China ina furaha kushiriki kwenye ujenzi wa miundombinu ya Uganda kupitia uwekezaji, ufadhili, na uungaji mkono wa kiufundi. Kuna msemo maarufu wa Kichina usemao 'Ili kuwa tajiri, jenga barabara kwanza'." Zhang amesema.

Zhang ameongeza kuwa kampuni za China zinazojenga miradi ya miundombinu si tu kwamba zinazalisha nafasi za ajira bali pia zinaendelea kuhamisha maarifa na ujuzi kwa jamii za wenyeji.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Uganda Katumba Wamala amesema barabara hiyo iliyopandishwa kiwango itapunguza muda wa kusafiri kati ya kaskazini na kati ya Uganda kwa masaa, ikiwezesha biashara na kuhimiza mafungamano ya kimikoa.

"Muda wa kusafiri utapungua kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo ni muhimu kwa jumuiya ya wafanyabiashara. Kadiri wanavyotumia muda mrefu barabarani, ndivyo wanavyopoteza pesa nyingi," Katumba amesema.

Li Changgui, naibu meneja mkuu wa CRBC, ameahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati ili kusaidia kufungua sifa bora za sehemu hiyo na kuhimiza ukuaji wa kijamii na kiuchumi.

China imefadhili miradi kadhaa mikubwa ya barabara nchini Uganda, ukiwemo mradi kinara wa Barabara Kuu ya Kampala-Entebbe, ambayo inaunganisha mji mkuu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe, lango kuu la nchi hiyo kwa dunia. 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Uganda Katumba Wamala akizungumza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa uboreshaji barabara ya Kayunga-Bbaale-Galiraya mjini Kayunga, Uganda, Julai 11, 2025. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Uganda Katumba Wamala akizungumza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa uboreshaji barabara ya Kayunga-Bbaale-Galiraya mjini Kayunga, Uganda, Julai 11, 2025. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha