

Lugha Nyingine
China yaripoti kuongezeka maradufu kwa watalii wa kigeni wakati likizo ya majira ya joto ikianza
Abiria wanaoingia China wakiwa wamepanga foleni kukaguliwa nyaraka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chongqing Jiangbei mjini Chongqing, kusini-magharibi mwa China, Julai 8, 2025. (Xinhua/Huang Wei)
BEIJING - China inashuhudia ongezeko kubwa la watalii wa kigeni wanaowasili wakati likizo ya majira ya joto inapoanza, huku watalii hao wakivutiwa na mfungamano wa kipekee wa utamaduni wa kale na hamasa ya mambo ya kisasa ya nchi hiyo.
Thomas Watts, mtayarishaji wa video fupi kutoka Marekani, anasema aliwaalika marafiki zake kwenda Chongqing majira haya ya joto baada ya kuona machapisho mengi mtandaoni yanayoonyesha miinuko mikali ya mji huo na hali motomoto.
"Inanikumbusha San Francisco, lakini kwa chakula cha pilipili kali zaidi na majengo marefu yenye taa za mwanga wa kuvutia. Nimekuja kujionea na kupiga video mwenyewe," amesema.
Hayuko peke yake katika kuichagua China kama eneo la kutembelea wakati wa majira haya ya joto. Kittiphume Pannil, mwanafunzi wa chuo kikuu kutoka Thailand, amewasili China kwa mara ya kwanza wiki iliyopita na anapanga kutumia mapumziko yake ya majira ya joto kwenye programu ya mawasiliano katika chuo kikuu kimoja cha mjini Chongqing.
"Nilipoiona Chongqing kutoka kwenye ndege, ilionekana kama mji wa taa zinazong'aa na majengo marefu, kama kitu kinachotoka siku za baadaye," Pannil amesema.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa katika nusu ya kwanza ya 2025, vituo vya mpakani vya Chongqing vilipokea wasafiri zaidi ya milioni 1.14 wanaoingia na kutoka, ongezeko la asilimia 35 kuliko mwaka jana wakati kama huo. Miongoni mwao, zaidi ya 330,000 walikuwa raia wa kigeni, ikiweka rekodi mpya kwa mji huo.
Mji mkuu wa nchi hiyo pia unavutia idadi inayoongezeka ya watembeleaji wa kimataifa ambapo kwa mujibu wa takwimu rasmi, bandari za Beijing zilihudumia wasafiri zaidi ya 640,000 wanaoingia na kutoka kuanzia Julai 1 hadi 10, wakiwemo watalii wa kigeni 171,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.1 kuliko mwaka jana wakati kama huo.
Miji mingine mikubwa ya China pia inapokea idadi kubwa ya wageni wa kimataifa ya kuweka rekodi.
Kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu rasmi, wasafiri wa kigeni jumla ya milioni 2.56 waliingia China kupitia viwanja vya ndege vya kimataifa vya Pudong na Hongqiao vya Shanghai katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 44.7 kuliko mwaka jana wakati kama huo.
Ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka, mamlaka za uhamiaji katika vituo vikuu vya mpakani zimeanzisha hatua mbalimbali ili kupunguza muda wa kusubiri na kuboresha uzoefu wa wasafiri.
Ongezeko hili la watalii wanaoingia China msimu huu wa joto si jambo lisilotarajiwa. Majira ya joto kwa kawaida huwa ni msimu wa likizo kuu kwa wasafiri kutoka Ulaya, Amerika Kaskazini na Asia Kusini-Mashariki, na ikisababisha watu wengi kuchagua China kama mahali wanapopendelea kutembelea katika miezi hii.
Ongezeko hilo pia limesababishwa na China kuendelea kulegeza sera za kuingia kwa watalii wa kigeni. Hadi kufikia sasa, sera ya China kukaa nchini humo kwa saa 240 bila visa kwa abiria wa kigeni wanaobadili ndege kwenda nchi nyingine inatumika kwa nchi 55, huku raia kutoka nchi 47 wanastahiki kuingia bila visa kwa upande mmoja.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma