

Lugha Nyingine
Biashara ya nje ya China yaonesha uhimilivu licha ya changamoto za kimataifa
BEIJING - Biashara ya nje ya China iliendelea kuimarika katika nusu ya kwanza ya 2025, huku uagizaji bidhaa kutoka nje ukirejea katika ukuaji mwezi Juni, wakati ambapo nchi hiyo yenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani ikionyesha uhimilivu licha ya hali za kutokuwa na uhakika kiuchumi duniani, takwimu kutoka Mamlaka Kuu ya Forodha ya China (GAC) zilizotolewa jana Jumatatu zinaonyesha.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa jumla ya biashara ya uagizaji na uuzaji nje bidhaa ya nchi hiyo kwa kipimo cha yuan iliongezeka kwa asilimia 2.9 katika kipindi cha Januari hadi Juni kufikia yuan trilioni 21.79 (dola za Kimarekani kama trilioni 3.05), rekodi ya juu kwa kipindi hicho.
Kwa mujibu wa GAC, kiwango hicho cha ukuaji kiliongezeka kutoka asilimia 2.5 lililorekodiwa katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka.
Akielezea ufanisi huo wa nusu ya kwanza wa biashara ya nje ya China kama "uliopatikana kwa kazi ngumu," Naibu Mkuu wa GAC Wang Lingjun amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing kwamba China bado inakabiliwa na kuongezeka kwa hatua za upande mmoja na kujilinda kibiashara duniani, ambayo imeongeza ugumu na hali ya kutokuwa na uhakika kwa mazingira ya nje.
Amesisitiza kuwa "juhudi kubwa" zinahitajika kudumisha ukuaji wa biashara ya nje katika nusu ya pili ya mwaka.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mauzo ya nje ya China yalipanda kwa asilimia 7.2 kuliko mwaka jana wakati kama huo katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, wakati uagizaji bidhaa kutoka nje ulishuka kwa asilimia 2.7.
Mwezi Juni pekee, takwimu hizo zinaonyesha kuwa mauzo ya nje ya nchi hiyo yalipanda kwa asilimia 7.2 kutoka mwaka uliopita, huku uagizaji bidhaa kutoka nje ulipata asilimia 2.3, ukibadilika kutoka mwelekeo wa kushuka kwa asilimia 2.1 mwezi Mei.
Takwimu hizo pia zimeonyesha kuboreka kimuundo kunakoendelea katika biashara ya nje ya China.
Mauzo ya bidhaa za teknolojia ya hali ya juu yalidumisha ukuaji mkubwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, yakipanda kwa asilimia 9.2 kuliko mwaka jana wakati kama huo, na hasa, chapa za China zilichukua sehemu kubwa ya jumla, zikifikia asilimia 32.4.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa, kwa upande wa washirika wa kibiashara, biashara kati ya China na ASEAN ilifikia yuan trilioni 3.67, ongezeko la asilimia 9.6, huku biashara kati ya China na Umoja wa Ulaya ikipanda kwa asilimia 3.5 na kufikia yuan trilioni 2.82. Aidha, biashara kati ya China na Marekani ilipungua kwa asilimia 9.3 hadi yuan trilioni 2.08.
Biashara kati ya China na nchi washirika wa Ukanda Mmoja, Njia Moja ilipanda kwa asilimia 4.7 hadi kufikia yuan trilioni 11.29, na biashara na nchi za Afrika iliongezeka kwa asilimia 14.4 hadi yuan trilioni 1.18 katika kipindi hicho.
Wang amesema kuwa China ina nguvu, imani na uwezo wa kushinda hatari na changamoto mbalimbali, akirejelea masoko yake mbalimbali na tulivu, bidhaa za uvumbuzi na zenye uwezo wa kushindana, na wauzaji bidhaa nje wenye uhimilivu kama kinga kuu dhidi ya hatari za nje.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma