Wataalamu na maafisa wa afya wakutana Uganda kwa ajili ya kutokomeza VVU, hepatitis B na kaswende barani Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 22, 2025
Wataalamu na maafisa wa afya wakutana Uganda kwa ajili ya kutokomeza VVU, hepatitis B na kaswende barani Afrika
Washiriki wakihudhuria Mkutano wa Kutokomeza Magonjwa Matatu Barani Afrika 2025 (Triple Elimination Conference in Africa 2025) mjini Kampala, Uganda, Julai 21, 2025. (Picha na Patrick Onen/Xinhua)

KAMPALA - Wataalamu, watunga sera, na watafiti wa sekta ya afya wameanzisha Mkutano wa Kutokomeza Magonjwa Matatu Barani Afrika 2025 (Triple Elimination Conference in Africa 2025) utakaofanyika kwa siku tatu mjini Kampala, mji mkuu wa Uganda, ili kuongeza kasi ya kutokomeza maambukizi ya VVU, kaswende na homa ya ini B kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto barani Afrika.

Mkutano huo unaofanyika chini ya kaulimbiu ya "Hatua Unganishi, Kuugeuza Mustakabali: Kutokomeza Magonjwa Matatu Barani Afrika ifikapo 2030," unaelezwa kuwa mkutano wa kwanza kabisa wa ngazi ya juu barani Afrika kuhusu kutokomeza maambukizi ya magonjwa matatu ya VVU, kaswende na homa ya ini B kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni akiwakilishwa na Makamu wa Rais Jessica Alupo amesisitiza umuhimu wa umoja na uvumbuzi katika kukabiliana na changamoto za kiafya za bara hilo hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya vipaumbele vya afya duniani na kupungua kwa ufadhili.

"Kama Afrika, na kama jumuiya ya kimataifa, lazima tuchukue hatua kwa umoja, uvumbuzi, na madhumuni ili kusukuma mbele afya ya mama na mtoto na kutokomeza maambukizi ya VVU, kaswende na homa ya ini B kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto," amesema Museveni.

Amesema kuwa magonjwa ya mlipuko yanayohusiana ya VVU, kaswende na homa ya ini B yanaleta mzigo mkubwa kwa afya ya jamii, hasa kupitia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua na kunyonyesha.

Waziri wa Afya wa Uganda Ruth Aceng amesema kuwa ingawa maendeleo yamepatikana katika kuzuia VVU, matunzo na matibabu, changamoto kubwa zinaendelea, haswa katika kushughulikia kaswende na homa ya ini B.

Amesema hadi kufikia mwisho wa mwaka 2024, Afrika ilikuwa na watu takriban milioni 26.3 wanaoishi na VVU, ikichukua asilimia 65 ya jumla ya watu wote duniani. Amesema, wakati huo huo, visa vya kaswende vinaongezeka duniani kote, huku watu wazima milioni nane wakiwa wameambukizwa, watu 700,000 walizaliwa na ugonjwa huo, na vifo 230,000 kwa mwaka.

Ameongeza kuwa, wakati Afrika imerekodi ongezeko kubwa zaidi la visa vya kaswende duniani, huku Botswana na Namibia pekee kwa sasa zikiwa kwenye njia ya kumaliza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, watu milioni 65 kote barani Afrika wameambukizwa homa ya ini B, ikichukua asilimia 63 ya maambukizi yote mapya duniani.

“Mafungamano ndiyo njia ya kuelekea sasa, hasa katika zama hizi za changamoto za ufadhili wa kifedha ambazo hazijawahi kutokea, ambapo tayari tunashuhudia punguzo katika fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo,” amesema Aceng.

Kwa mujibu wa waandaaji, mkutano huo unaendana na malengo ya kutokomeza magonjwa ya Shirika la Afya Duniani ya 2030 na Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika, ambazo zote zina dira ya Afrika yenye afya na himilivu zaidi. ■

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha