Waziri Mkuu wa Tanzania ataka mipango ya kuwa na zana za kisasa za kilimo

(CRI Online) Agosti 05, 2025

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo nchini humo kuanzisha mfumo utakaowezesha taasisi za kilimo kupata zana za kisasa za kilimo, hatua inayolenga kuboresha uzalishaji na kufanya mageuzi katika sekta hiyo.

Akizungumza katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo yanayoendelea mjini Dodoma, Bw. Majaliwa amesisitiza kuwa taasisi za kilimo zinaweza kuboresha mavuno kama zikiwa na teknolojia za kisasa.

Amependekeza kuwa Wizara ya Kilimo inapaswa kufikiria kutoa mashine kwa mkopo ili kuwezesha upatikanaji, kutokana na gharama kubwa za vifaa vya kilimo cha kisasa, ikiwemo mashine za uvunaji na vifaa vya umwagiliaji.

Majaliwa amesema, wakati wa msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024 na 2024/2025, vifaa vya kilimo vyenye thamani ya shilingi trilioni moja za Tanzania viligawiwa kwa wakulima, na tani milioni 3.8 za mazao zenye thamani ya shilingi trilioni 6.2 ziliuzwa kupitia mashirikisho ya wakulima.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha