UM wasema Uganda kupokea wakimbizi milioni 2 ifikapo mwisho wa mwaka 2025

(CRI Online) Agosti 05, 2025

Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema, wakimbizi milioni 1.93 wanaishi nchini Uganda hivi sasa, na idadi hiyo huenda ikafikia milioni 2 ifikapo mwisho wa mwaka 2025 kutokana na kuongezeka kwa migogoro nchini Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Farhan Haq amesema hayo jana Jumatatu alipokutana na wanahabari na kuongeza kuwa, sera inayoendelea ya nchi hiyo kuhusu wakimbizi inawaruhusu kuishi, kufanya kazi na kupata huduma za umma, lakini upungufu wa ufadhili unaathiri sana utoaji wa misaada na kutishia kuharibu matokeo yaliyopatikana katika miaka mingi iliyopita.

Ameongeza kuwa, hivi sasa ufadhili kwa wakimbizi nchini Uganda ni wa asilimia 25 tu, na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) linatoa wito wa msaada wa haraka na endelevu wa kimataifa ili kuhakikisha wakimbizi na jamii zao wanaweza kuishi maisha salama na yenye heshima zaidi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha