Rais wa Sudan Kusini na mkuu wa majeshi wa Uganda wafanya mazungumzo kuhusu usalama

(CRI Online) Agosti 11, 2025

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba wamekutana na kufanya mazungumzo mjini Juba kuhusu kuimarisha utulivu wa kikanda.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Uganda, inasema kwenye mkutano huo uliofanyika jumamosi, Rais Kiir aliipongeza Uganda kwa mchango wake katika kudumisha amani nchini Sudan Kusini.

Uganda imetuma wanajeshi nchini Sudan Kusini kwa ombi la serikali ya Sudan Kusini, kufuatia mapigano kati ya vikosi vya waasi na wanajeshi wa serikali. Jenerali Kainerugaba amesema Uganda itaendelea kuimarisha uhusiano na Sudan Kusini.

Baada ya kukutana na Rais Kiir, Jenerali Kainerugaba alitembelea makao makuu ya “Operesheni Mlinzi Wa Kimya”, ambapo alikutana na wanajeshi wa Uganda na makamanda wanaosimamia ujumbe huo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha