Mtu wa 4 aokolewa kwenye ajali ya kuporomoka kwa mgodi wa dhahabu nchini Tanzania

(CRI Online) Agosti 14, 2025

Vikosi vya uokoaji vya Tanzania vimefanikiwa kumwokoa fundi mwingine wa uchimbaji madini kutoka kwenye machimbo ya dhahabu yaliyoporomoka mkoani Shinyanga, na kufanya idadi ya jumla ya watu walionusurika kufikia wanne, na wengine 21 bado hawajapatikana.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Bw. Julius Mtatiro amesema fundi huyo aliyeokolewa alikutwa katika hali mbaya na bado hakuna uhakika kuhusu hali ya watu 21 waliokwamwa chini ya kifusi.

Naibu waziri wa madini Bw. Steven Kiruswa amesema kazi za uokoaji ikiongozwa na vikosi vya ulinzi na usalama inaendelea usiku na mchana.

Ajali hiyo ilitokea Jumatatu katika mgodi wa dhahabu wa Wachapakazi wakati wa ukarabati wa mabomba chini ya ardhi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha